BAADHI YA WADAU WASHIKILIA MSIMAMO WA KUFUTILIWA MBALI MTAALA WA CBC.


Jopokazi la kuangazia utekelezwaji wa mtaala mpya wa elimu CBC linapoendeleza vikao vya kukusanya maoni kuhusu mtaala huo kutoka kwa wakenya maeneo mbali mbali ya nchi, wadau mbali mbali wameendelea kushinikiza kufanyiwa marekebisho makubwa mtaala huo la sivyo uondolewe kabisa.
Wa hivi punde kutolea hisia utekelezwaji wa mtaala huo ni mwakilishi wa kike katika kaunti hii ya Pokot magharibi Rael Kasiwai ambaye alisema kwamba wanafunzi katika maeneo mengi ya nchi ikiwemo kaunti hii hawataweza kunufaika na mtaala huo iwapo utatekelezwa jinsi ulivyo kwa sasa.
Alisema mtaala wa CBC ni ghali mno kutokana na mahitaji mengi ambayo yanaambatana nao na hali ya umasikini miongoni mwa wazazi wengi haiwaruhusu kuumudu.
“Mtaala huu ni mzuri ila kwa kaunti kama hii ya Pokot magharibi tuna changamoto nyingi. Wazazi wengi hawawezi kuumudu kutokana na mahitaji mengi ya kifedha yanayoambatana nao. Vitu vingi ambavyo vinahitajika kununuliwa na wazazi vinaufanya kuwa ghali mno kwa mzazi.” Alisema Kasiwai.
Kasiwai alitaka uamuzi wa kutekelezwa mtaala huo kuangaziwa upya.
“Kwa hivyo tunasema masomo ya CBC hayatafanya kazi kwa kaunti zote. Wanaoshinikiza mtaala huu kutekelezwa wanafaa kutafakari upya uamuzi wao.” Alisema.
Wakati uo huo Kasiwai aliitaka serikali kuangazia upya swala la uhamisho wa walimu kwani limechangia pakuba kusambaratika ndoa za walimu wengi akipendekeza walimu kufunza maeneo walikozaliwa ili kufanya rahisi kazi zao.
“Uhamisho wa walimu umeharibu familia nyingi za walimu. Pia mwalimu kupelekwa sehemu ambako haelewi lugha ya wenyeji pale inaleta shida kidogo kwa maswala ya uongozi. Kwa hivyo kama wabunge tumepitisha kwa kauli moja kwamba walimu wote wafunze walikozaliwa ili kazi yao iwe rahisi.” Alisema.