BAADHI YA VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WATILIA SHAKA UHALALI WA MATOKEO YA MTIHANI WA KITAIFA KCSE.
Siku chache tu baada ya matokeo ya mtihani wa kitaifa kwa kidato cha nne KCSE kutangazwa rasmi aliyekuwa seneta wa kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ametilia shaka matokeo hayo akitaka uchunguzi kuendeshwa kubaini kilichotokea.
Kulingana na Poghisio, matokeo hayo ambayo yalitangazwa na waziri wa elimu Ezekiel Machogu hayaleti picha kamili ya jinsi wanafunzi hao walifanya ikilinganishwa na miaka ya awali akidai huenda kulishuhudiwa udanganyifu mkubwa katika mtihani huo.
“Imekuwa tatizo kutambua iwapo matokeo hayo yalikuwa halali au mitihani iliibwa kwa sababu utakuta sehemu nyingine nchini watoto wamepita zaidi kuliko hali ya kawaida. Kwa mfano kuna shule ambayo kuna alama ya A na kisha kila mtu anapata B. Hiyo si kawaida, hivyo uchunguzi unapasa kuendeshwa kubaini kilichotokea.” Alisema Poghisio.
Aidha Poghisio alitaka uchunguzi huo kutoendeshwa na wadau katika sekta ya elimu bali idara za uchunguzi akisisitiza kwamba huenda elimu nchini Kenya ikakosa umuhimu iwapo mkondo wa wizi wa mitihani ya kitaifa utaendelea katika shule za hapa nchini.
“Wizi wa mitihani ni uhalifu na sijui ni kwa nini hawahusishi watu wa idara za uchunguzi kama polisi na CID katika uchunnguzi huo. Huwezitumia walimu ambao walikuwa pale au baraza la mitihani kufanya uchunguzi huo ni lazima watu wanaojua kufanya uchunguzi watumike.” Alisema.
Wakati uo huo Poghisio alilalamikia matokeo duni katika mitihani ya kitaifa kwenye shule za kaunti hii ya Pokot magharibi akielezea haja ya viongozi katika kaunti hii kufanya kikao na wadau katika sekta ya elimu kufahamu chanzo cha hali hii.
“Tutafuatilia kama viongozi wa Pokot magharibi tufahamu ni kwa nini wanafunzi hawafanyi vyema katika mitihani hiyo. Tutafanya kikao na wadau tufahamu tatizo liko wapi.” Alisema.