BAADHI YA VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WAPUUZILIA MBALI KUBUNIWA CHAMA KIPYA.


Baadhi ya viongozi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameendelea kupuuzilia mbali madai ya kubuniwa chama kipya katika kaunti hii kinachonuiwa kutumika katika uchaguzi mkuu ujao.
Mwakilishi wadi maalum Elijah kasheusheu amesema kuwa hamna mkutano wowote ambao umeandaliwa na viongozi katika kaunti hii ya pokot magharibi na kuafikiwa maelewano ya kubuni chama kipya kando na vyama vya KANU na Jubilee na sasa UDA.
Akizungumza na kituo hiki, Kasheusheu anasema sasa si wakati wa kubuni vyama vya kikabila, bali kuangazia siasa ambazo zitawaunganisha wananchi wote.
Aidha kasheusheu ametoa wito kwa wakazi wa kaunti hii kutokubali kushawishiwa kujiunga na chama chochote kitakachobuniwa kwa madai kuwa ni chama cha jamii ya pokot, na badala yake kuendelea kuunga mkono vyama vyenye sera za kumnufaisha mwananchi.