BAADHI YA VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WAPINGA MATUMIZI YA NPR KATIKA KUIMARISHA USALAMA.


Licha ya shinikizo za baadhi ya viongozi kutoka bonde la kerio kutaka uajiri wa maafisa zaidi wa NPR, mbunge wa Kapenguria katika kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Moroto ameelezea kutokuwepo haja ya uajiri wa maafisa hao.
Akizungumza na kituo hiki Moroto alisema kwamba uajiri wa maafisa hao hautaleta suluhu lolote la utovu wa usama eneo la bonde la kerio kwani kulingana naye wahalifu hujificha nyuma ya maafisa hao kuendeleza uovu.
Moroto sasa anaitaka serikali kuwatuma maafisa zaidi polisi katika eneo hili ili kukabiliana na wizi wa mifugo ambao ndicho chanzo kikuu cha utovu wa usalama bonde la kerio.
“Hata haya mambo ya NPR vile watu wanazungumza hapa hivi haina maana kwa kwa sababu wakora wananunua bunduki na kujificha nyuma ya NPR. Sasa maafa yakitokea watu wanaanza kulaumu kwamba ni NPR wamesababisha na kumbe ni wahalifu kwa sababu hakuna tofauti ya mlio wa risasi ya NPR na ya mkora.” Alisema Moroto.
Wakati uo huo Moroto alitaja migawanyiko ya kisiasa miongoni mwa wakazi na viongozi kuwa chanzo kikuu cha utovu wa usalama maeneo haya akidai baadhi ya viongozi wa kisiasa nchini wanachochea hali hiyo.
“Mambo ya usalama maeneo haya yalikuwa yametulia lakini ni mwaka huu tu ndo yameanza ni kwa sababu ya matamshi ambayo yanatoka kwa watu ambao wamechaguliwa juzi. Kenya hii sasa imegawana, kuna watu wa azimio na Kenya kwanza na utapata wale wengine wanachochea watu.” Alisema.