BAADHI YA VIONGOZI BARINGO WATAKA MARUFUKU YA KUTOKUWA NJE KUONDOLEWA


Viongozi eneo la Baringo kaskazini kaunti ya Baringo wameitaka serikali kuondoa marufuku ya siku 30 ya kutokuwa nje nyakati za usiku ambayo iliwekwa takriban mwezi mmoja uliopita.
Wakiongozwa na mwaniaji kiti cha ubunge eneo hilo Joseph Makilap viongozi hao wamedai kuwa marufuku hiyo ingetekelezwa eneo bunge la Tiati ambako wanadai ni makao ya wahalifu wanaosababisha ukosefu wa usalama katika bonde la kerio.
Wamepuuzilia mbali mikakati hiyo ya serikali wakisema kuwa imepelekea wakazi wengi wa maeneo hayo kuhangaika huku wahalifu wanaolengwa wakijificha maeneo ya misitu.
Serikali ilitoa agizo la kutokuwa nje mwezi mmoja uliopita kwenye baadhi ya maeneo ya kaunti za Pokot magharibi, Baringo na Elgeyo Marakwet ili kuendeleza msako dhidi ya wahalifu pamoja na kutwaa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria miongoni mwa wakazi.
Mshirikishi wa serikali eneo la bonde la ufa Mohammed Maalim alisema kuwa mauaji na wizi wa mifugo yameendelea kushuhudiwa katika bonde la kerio licha ya mikutano ya Amani ambayo imekuwa ikiendelezwa na wakuu wa usalama, wazee pamoja viongozi wa kidini.
Baadhi ya wakazi maeneo hayo pia wamelalamikia agizo la kutokuwa nje wakisema limeathiri pakubwa shughuli za kawaida hasa maeneo ya mashinani.
Mamia ya wakazi wameuliwa katika bonde la kerio tangu mwanzoni mwa mwaka huu, wengine wakipoteza makazi yao, huku maelfu ya mifugo wakiibwa na wahalifu.