BAADHI YA SHULE ZA MSINGI KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI ZINAKUMBWA NA UHABA WA WALIMU


Huku ikiwa ni wiki ya pili tangu masomo kurejelewa humu nchini na wanafunzi kurejea shuleni siku ya jumatatu wiki jana, baadhi ya shule zinapitia changamoto si haba kutokana na uhaba wa walimu.
Kulingana na mbunge wa Kapenguria kaunti hii ya Pokot Magharibi Samuel Morot ni kuwa baadhi ya shule zina wanafunzi zaidi ya 500 na zinahudumiwa na walimu watatu pekee yao.
Akizungumza na wanahabari alipoitembelea shule ya msingi ya Sabina iliyoko Sook, Moroto amesema kuwa baadhi ya shule ambazo ni za serikali zimesalia nyuma huku akisema kuwa ni vigumu kwa wanafunzi hao kupata elimu sawa na wanafunzi wengine.
Moroto aidha ametoa wito kwa wakuu wa elimu kwenye kaunti hii ya Pokot Magharibi kutembelea shule hiyo ili kuhakikisha kwamba hali hiyo inaangaliwa kwa umakini.