AZIMIO YAWASILISHA RUFAA YA KUPINGA MATOKEO YA UCHAGUZI WA URAIS.


Chama cha muungano wa azimio la umoja one Kenya hatimaye kimewasilisha rufaa ya kupinga matokeo ya uchguzi mkuu wa agosti 9.
Katika stakabadhi yenye kurasa 76, kinara wa muungano huo Raila Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karua, wameibua maswala 26 ya kutilia doa mchakato mzima wa uchaguzi wa agosti 9.
Maswala makuu yaliyoibuliwa ni kama vile kuingiliwa kwa mfumo wa kielektroniki wa wapigaji kura katika mitambo ya KIEMS, makamishina wanne wa IEBC kujitenga na matokeo, ukosefu wa kuhakiki na kutangaza kura za maeneo bunge 27 na dosari katika rekodi za kura za fomu za 34a, 34b na 34c.
Muungano wa azimio ulidai kuwa fomu hizo zimekuwa zikifutwa na kubadilishwa kila mara kwenye wavuti wa IEBC tangu uchaguzi ulipofanyika.
Kupitia wakili Paul Mwangi Raila na Karua walidai kwamba mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alikiuka mwongozo wa uchaguzi kwa mujibu wa kesi ya Maina Kiai.
Wanashinikiza mahakama ya juu kumtangaza Chebukati kuwa afisa mhuni asiyefaa kusimamia uchaguzi nchini hivyo kupendekeza tume nyingine kubuniwa ili kuendesha marudio ya uchaguzi iwapo ombi lao litafaulu.
Aidha azimio ilisema kuna utata katika usahihi wa asilimia ya wapiga kura waliojitokeza na kwamba IEBC ilijikanganya kwa kusema waliojitokeza walikuwa asilimia 52 na kisha baadaye kuripoti asilimia 65.4.
Hata hivyo azimio inasema matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na Chebukati ni tofauti kabisa na idadi ya wapiga kura walioripotiwa kujitokeza na kwamba kuna kura takriban alfu 250 ambazo hazijulikani zilikotoka.
Aidha inadaiwa Ruto hakupata asilimia 50 na kura moja ya ziada jinsi inavyohitajika ili kutangazwa kuwa mshindi na hivyo kushinikiza uhesabu wa kura kurudiwa na kisha Raila kutangazwa kuwa mshindi.
Vile vile muungano wa azimio unadai kuwa IEBC ilishindwa kulinda vifaa vya uchaguzi na hata kuwaruhusu raia watatu wa Venezuela kuingilia mitambo yake ya KIEMS kuhitilafiana na kura na hata kutatiza asilimia ya waliojitokeza.
Wanasema wana ushahidi ambao unaonyesha mitambo ya IEBC ikidukuliwa kuanzia mwezi machi na kwamba mchakato mzima wa uchaguzi ulikumbwa na udanganyifu.