Athari za ajali ya ndege Kaben zadhihirika mwaka mmoja baadaye

Aliyekuwa mkuu wa majeshi nchini jenerali Francis Ogolla, Picha/Maktaba
Na Benson Aswani
Mwaka mmoja tangu kuanguka ndege iliyomuua aliyekuwa mkuu wa majeshi nchini jenerali Francis Ogolla, wakazi wa kijiji cha Kaben mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo Marakwet ilikotokea ajali hiyo bado wanaishi na makovu ya kile walichoshuhudia.
Katika ajali hiyo iliyotokea Alhamisi tarehe 18 mwezi Aprili mwaka 2024, Jenerali Francis Ogolla alifariki dunia pamoja na maafisa wengine tisa waliokuwa ndani ya helikopta ya jeshi iliyokuwa na maafisa 11 wa KDF dakika chache baada ya saa tisa alasiri.
Maafisa hao walikuwa wakitoka katika ziara ya kikazi katika shule ya sekondari ya wavulana ya Cheptulel, Pokot Magharibi ambako walihudhuria mkutano kwa saa moja.
Mwaka mmoja baadaye shughuli zinaonekana kuathirika eneo hilo, shamba la Sindar ambako ndege hiyo ilianguka, kwa kawaida likiwa na shughuli nyingi, sasa linaonekana kutelekezwa.
“Watu waliokuwa wakifanya kazi katika shamba hili wametawanyika. Ukiwauliza mbona siku hizi hamfanyi kazi hapa kama awali, wanasema kitu waliona katika mkasa wa ndege hiyo hawajawahi kukiona. Nadhani walishtuka sana kutokana na kisa hicho,” alisema mkazi mmoja.
Inaarifiwa wakazi waliokuwa wakihudumu katika shamba hilo walipatwa na mshutuko kutokana na kile walichoshuhudia, baadhi wakielezea haja ya serikali kuingilia kati ili kuwapa wakazi hao msaada utakaowawezesha kurejelea hali yao ya kawaida.
“Tangu siku hiyo kuna watu ambao hawajahi kwenda tena shambani. Ukiwaambia twende tufanye kilimo, wanasema huenda kisa hicho cha ajali ya ndege kikatokea tena. Kwa hivyo serikali inapasa kuwapa msaada wakazi hawa na hata kuwapa ushauri nasaha ili warejelee hali yao ya kawaida,” alisema.
Naibu chifu kata ndogo ya Kaben Isaac Murkomen anasema kabla ya kutokea ajali hiyo jamii ya eneo hilo kutoka pande za Pokot na Marakwet ilikuwa imeungana kuendeleza mradi wa kilimo katika shamba hilo la Sindar, kama njia moja ya kudumisha amani, ila sasa mradi huo ulikwama.
“Shamba hili la Sindar lilikuwa likitumika wakati huo kama mradi wa kuleta amani kati ya jamii za Pokot na marakwet. Wananchi kutoka pande zote mbili walikuwa wamekuja pamoja kuendeleza kilimo. Lakini tangu ajali hiyo ya ndege, shamba hili limetelekezwa na hamna shughuli yoyote inayoendelea hapa,” alisema Murkomen.
Timu ya wachunguzi ambayo wizara ya ulinzi ilikabidhi jukumu la kubaini chanzo cha ajali ya helikopta ilihitimisha kuwa ilisababishwa na hitilafu ya injini.
Ripoti hiyo, ambayo ilikabidhiwa rais William Ruto mnamo Ijumaa, Aprili 12, ilihitimisha kuwa ajali hiyo ya ndege ilitokea baada ya helikopta ya Bell Huey (KAF 1501) kupata matatizo ya injini hewani.