ARAULE ATAKA KUIMARISHWA BARABARA YA SUNFLOWER HADI UWANJA WA NDEGE


Mwakilishi wadi ya Mnagei eneo bunge la Kapenguria kaunti hii ya Pokot magharibi Benjamin Araule ameahidi kuhakikisha hali ya barabara ya kutoka shule ya Sunflower mjini Makutano hadi kiwanja ndege inaimarishwa.
Araule amesema kuwa barabara hiyo ni moja ya bara bara ambazo ziko chini ya mji wa Makutano na pia inatumika na watu wengi hivyo hali yake inafaa kuimarishwa, akiahidi kukutana na mbunge wa Kapenguria Samwel moroto katika juhudi za kuhakikisha hilo linafanikishwa.
Wakati uo huo Araule amemtaka gavana wa kaunti hii John Lonyangapuo pamoja na mwenyekiti wa kamati ya bunge la taifa kuhusu barabara David Pkosing kuiweka barabara hiyo kuwa miongoni mwa barabara ambazo zinastahili kuimarishwa.
Araule alikuwa akizungumza baada ya mkutano na mamlaka ya barabara kuu nchini KENHA uliotumika kupanga ujenzi wa barabara ya kutoka mjini Kitale kaunti ya Trans nzoia hadi Morpus ili kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikitokea hasa eneo la kamatira.
Ni shughuli ambayo itachukua miaka mitatu kukamilika anavyoeleza naibu mkurugenzi wa maendeleo katika mamlaka hiyo mhandisi John Dinika.