ALEUTUM: VISA VYA UTOVU WA USALAMA VIMEPUNGUA KWA ASILIMIA MOJA PEKEE POKOT MAGHARIBI TANGU KUANZA OPARESHENI DHIDI YA WAHALIFU.

Mwakilishi kina mama katika kaunti ya Pokot magharibi Rael Aleutum amesema kwamba visa vya utovu wa usalama maeneo ya mipaka ya kaunti hiyo vimepungua kwa asilimia ndogo sana tangu kuanza oparesheni ya kukabili wahalifu katika kaunti 6 za kaskazini mwa bonde la ufa.

Akizungumza siku mbili tu baada ya mtu mmoja kuuliwa eneo la Lami nyeusi mpakani pa kaunti hiyo na kaunti jirani ya Turkana, Aleutum alisema kwamba wahalifu hao sasa wamebadili mbinu ya kutekeleza mashambulizi ambapo sasa hawaibi tena mifugo na badala yake kutekeleza mauaji ya raia na kutoweka.

“Bado kuna utovu wa usalama kaunti hii na iwapo visa hivyo vimepungua basi ni kwa asilimia moja pekee. Japo kuja kwa waziri Kindiki kumeleta mabadiliko kidoko, ila sasa wahalifu hao wamebadili mbinu za kutekeleza uhalifu ambapo sasa wanachukua muda kidogo na kisha wanarejea kuuwa mtu.” Alisema Aleutum.

Aleutum alimtaka waziri wa usalama na maswala ya ndani ya nchi Kithure Kindiki kurejea eneo hilo na kuongoza kikao na viongozi kutoka kaunti zote za bonde la kerio, ili kwa pamoja wapate njia mwafaka ya kukabiliana na uhalifu huo ambao umegharimu maisha ya wananchi wengi.

“Wito wangu kwa waziri Kindiki ni kwamba, aje na afanye kikao na viongozi wote wa kaunti za bonde la kerio ili kwa pamoja tuweke mikakati ya jinsi ya kukabiliana na swala hili la utovu wa usalama.” Alisema.

Wakati uo huo Aleutum alipinga vikali pendekezo la kuhamishwa kambi ya jeshi ambayo ilitarajiwa kujengwa eneo la Chesogon hadi Kerio river, akisema kwamba hatua hiyo haitawafaa wengi wa wananchi wa kaunti hiyo kutokana na umbali wa eneo itakakojengwa.

“Waziri Kindiki alipokuja kaunti hii aliahidi kwamba kutajengwa kambi ya jeshi hapo Chesogon. Ila majuzi nimesikia kwamba inahamishwa hadi kerio river. Hatua ya kuhamishwa kambi hiyo haitatusaidia sisi wakazi wa pokot magharibi kwa sababu kerio river ni mbali sana. Hivyo swala hilo mimi nakataa.” Alisema.