AKINA MAMA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI WAOMBA KUUNGWA MKONO KATIKA SIASA
Wengi wa akina mama nchini wamekosa nafasi za uongozi katika ulingo wa kisiasa kutokana upinzani mkali kutoka kwa wenzao wa kiume.
Haya ni kulingana na aliyekuwa spika wa bunge la kaunti hii ya Pokot magharibi Catherine Mukenyang ambaye amesema wanasiasa wa jinsia ya kiume hushirikiana kuhakikisha kwamba akina mama hawapati nyadhifa zingine za uongozi hali ambayo imewafanya wengi wao kuwania tu wadhifa wa mwakilishi wa akina mama.
Mukenyang ambaye aliwania wadhifa wa mwakilishi wa akina mama kaunti hii katika uchaguzi mkuu uliopita bila mafanikio sasa anatoa wito kwa wenzao wa kiume kuwaunga mkono akina mama ili pia wapate nafasi zaidi za uongozi kando na ule wa mwakilishi akina mama.
Wakati uo huo Mukenyang ametoa wito kwa viongozi kaunti hii kusisitiza umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike akisema kwamba idadi kubwa ya watoto wa kike kaunti hii hasa eneo la Pokot kaskazini hawajapata nafasi ya kupata elimu kufuatia changamoto nyingi wanazopitia katika jamii ikiwemo ndoa za mapema na ukeketaji.