Agizo la kuwapiga risasi miguuni wanaovuruga amani kwenye maandamano lazidi kukeketa

Na Benson Aswani
Agizo la rais William Ruto kwa maafisa wa polisi kuwapiga risasi na kuwajeruhi miguuni wahalifu ambao wanatumia maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen-Z kuvuruga amani na kupora mali imeendelea kuibua hisia mbali mbali nchini.


Wa hivi punde kuzungumzia kauli hiyo ni mbunge wa Sigor kaunti ya Pokot Magharibi Peter Lochakapong ambaye ametetea kauli ya rais akisema kwamba inatafsiriwa vibaya na wakosoaji wake, akisisitiza kwamba rais Ruto alitoa kauli hiyo kulingana na katiba ya nchi.


Hata hivyo Lichakaponga aliwahimiza maafisa wa vitengo mbali mbali vya usalama nchini kutekeleza kazi zao kulingana na jinsi wameelekezwa na katiba.


“Wakati rais anapozungumza, anazungumza kwa mujibu wa katiba na kulingana na sheria zilizopo. Lakini watu hutafsiri vibaya. Lakini ninachofahamu ni kwamba rais hawezi kusema kitu ambacho ni kinyume cha katiba. Kwa hivyo mimi nasema tu kwamba vitengo vyetu vya usalama vifanye kazi zao kulingana na katiba,” alisema Lochakapong.


Kwa upande wake mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto alisema kwamba huenda rais hakumaanisha kile alichokisema ila kwa kuteleza ulimi, akiwahimiza viongozi na wananchi kutochukulia kwa uzito kauli hiyo na badala yake kuendelea kuheshimu uongozi wake.


“Mtu anaweza kusema mambo mengi, na haimaanishi kwamba yote anayosema ni mazuri. Kwa hivyo inapasa kuchukua tu yale ambayo ni mazuri na kusonga mbele. Kama vile rais alisema, ukipata mtu anataka kusumbua, twanga mguu. Hakusema wauawe. Hata hivyo ni ulimi uliteleza. Sasa ni kwa nini tunaifanya kuwa kitu kubwa zaidi,” alisema Moroto.