AGIZO LA KUTOSAJILI SHULE ZAIDI LASHUTUMIWA NA VIONGOZI POKOT MAGHARIBI
Hisia mseto zimeendelea kuibuliwa nchini kufuatia agizo la wizara ya elimu kwa maafisa wake kutosajili shule zaidi nchini.
Mwakilishi wadi ya Batei kaunti hii ya Pokot magharibi Solomon Ang’elei amekosoa agizo hilo akisema kuwa baadhi ya kaunti ikiwemo pokot magharibi zilisalia nyuma kwa miaka mingi na iwapo agizo hilo litatekelezwa basi litaathiri juhudi za wakazi wa kaunti hii kuwa sawa na wakenya wengine.
Angelei amesema zipo shule nyingi ambazo zimeanzishwa maeneo ya mipakani pa kaunti hii ya pokot magharibi kama njia moja ya kukabili utovu wa usalama kwa kuwawezesha wakazi wa maeneo hayo kupata elimu na iwapo hazitasajiliwa basi kutaendelea kushuhudiwa tatizo la usalama maeneo hayo.
Wakati huo Ang’elei amelalamikia uhaba wa walimu katika shule nyingi hasa maeneo ya mashinani kaunti hii akitoa wito kwa tume ya huduma za walimu TSC kuchukua hatua ya kutuma walimu zaidi katika shule hizo.