AFISA WA POLISI AZUILIWA KAPENGURIA KWA TUHUMA ZA KUJARIBU KUMBAKA MWANAFUNZI.


Afisa mmoja wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Kabichbich kaunti hii ya Pokot magharibi anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kapenguria kwa tuhuma za kujaribu kumbaka mwanafunzi wa darasa la saba.
Akithibitisha hayo OCS wa Kabichbich Anthony Mmaisi amesema kuwa uchunguzi dhidi ya afisa huyo utaendeshwa na hatua mwafaka kuchukuliwa kwa kwenda kinyume na maadili ya kazi yake kama afisa wa serikali.
Kulingana na Mmaisi afisa huyo ambaye ni mraibu wa pombe alikuwa amehudumu miezi miwili pekee tangu kuhamishiwa kituo hicho kutoka eneo la Kirinyaga.
Mkurugenzi wa elimu eneo la Lelan John Kitur amesema kuwa kisa hiki si cha kwanza kwa afisa huyo wa polisi kwani aliwahi kupatikana na kosa la kuishi na mwanafunzi akisema afisa huyo ni hatari kwa wakazi wa eneo hilo na kuwa huenda ana matatizo ya akili.