AFISA WA JESHI MUSTAAFU ATAKA MBINU YA KUWAKABILI MAJANGILI KUBADILISHWA.

Wadau mbali mbali katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kukosoa mbinu ambayo inatumika na serikali kukabili utovu wa usalama ambao umekuwa ukishuhudiwa hasa katika kaunti 6 za kaskazini mwa bonde la ufa.

Wa hivi punde kukosoa mbinu hiyo ni afisa mustaafu wa jeshi Kapteni Peter Mermer ambaye alisema kwamba serikali ingekumbatia matumizi ya wazee pamoja na maafisa wastaafu kuwatambua wahalifu hao kwani ndio walio karibu na wananchi na wanaofahamu historia ya maeneo haya.

Aidha Mermer alipendekeza kwa serikali kubuni kitengo cha maafisa wa usalama wastaafu kuangazia maswala ya usalama hasa maeneo ya vijijini jinsi ilivyo katika mataifa ya Uganda na Tanzania.

“Wazee wanajua historia ya jinsi hawa watu walikuwa wanaishi tangu zamani, jinsi ambavyo walikuwa wakisuluhisha mizozo kati yao. Hivyo wanafaa kutumika katika kutafuta suluhu kwa tatizo la usalama maeneo haya. Maafisa wa usalama wastaafu pia wanafaa kupewa nafasi ya kushughulikia swala hili.” Alisema Mermer.

Alitoa wito kwa waziri wa usalama Prof. Kithure Kindiki kuondoa maafisa wa jeshi katika oparesheni ya kuwakabili wezi wa mifugo katika kaunti hizo, na badala yake kuwaachia polisi pekee wakishirikiana na wazee pamoja na maafisa wastaafu anaosema wanafahamu vyema maeneo haya.

“Hii ni kazi ya polisi kwa sababu wao wamekaa na raia na wanafahamu vyema maisha ya hawa watu. Maafisa wa jeshi hawajui hali ya maisha ya raia na haya si majukumu ya jeshi. Naomba waziri Kindiki awaondoe maafisa wa jeshi na kuwapa nafasi polisi kwa ushirikiano na wazee pamoja na maafisa wastaafu kutafuta suluhu.” Alisema.

Wakati uo huo Mermer aliwapongeza viongozi wa kaunti hiyo kwa kile alisema kwamba juhudi zao kuhakikisha kwamba maeneo ya Turkwel na Ombolion yaliyokuwa yameorodheshwa miongoni mwa maeneo hatari yanaondolewa katika orodha hiyo.

“Nawapongeza viongozi wetu kaunti hii wakiongozwa na gavana pamoja na wabunge kwa kuhakikisha kwamba maeneo ya Turkwel na Ombolion yanaondolewa miongoni mwa maeneo ambayo yalikuwa yameorodheshwa kuwa hatari. “ alisema.