AFISA WA BODI YA KUAJIRI WAFANYIKAZI NA WAKILI WA KAUNTI WAHOJIWA.

Na Benson Aswani
Kamati ya bunge la kaunti ya Pokot magharibi kuhusu uteuzi imeendesha mchujo wa waliopendekezwa kuhudumu katika wadhifa afisa mkuu mtendaji wa bodi ya kuajiri wafanyikazi na wakili wa kaunti.
Akifika mbele ya kamati hiyo Consolata Chepchirchir Arusei ambaye amependekezwa katika wadhifa wa afisa mkuu mtendaji wa bodi ya kuajiri wafanyikazi amesema kuwa atatekeleza majukumu yake katika bodi hiyo kwa kuzingatia sheria na uhuru wa bodi hiyo bila kushawishiwa kisiasa iwapo ataidhinishwa kuhuduku katika wadhifa huo.
Arusei amesema kuwa atatekeleza majukumu yake kitaaluma kulingana na matakwa ya bodi hiyo na kuwa yuko tayari kuhudumu katika wadhifa huo kwa kipindi cha miaka sita.
Robert Katina ambaye ambaye amependekezwa kuhudumu katika wadhifa wa wakili wa kaunti alisema kuwa ujuzi wake katika Nyanja mbali mbali tangu alipoacha majukumu yake kama spika wa bunge hilo unampa fursa bora ya kutekeleza majukumu yake inavyostahili.
Aidha amesema kuwa atajitolea kikamilifu katika kutoa ushauri unaostahili kwa gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi katika juhudi za kuhakikisha kuwa huduma zinatolewa kulingana na sheria hitajika.