VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WATAKA BUNDUKI ZILIZOKABIDHIWA MAAFISA WA NPR KUTWALIWA.

Baadhi ya viongozi kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kuilaumu serikali kupitia wizara ya usalama wa ndani ya nchi kwa kuwakabidhi maafisa wa akiba NPR upande wa Elgeyo marakwet Bunduki na kuitenga kaunti hiyo.

Wa hivi punde kuzungumzia swala hilo ni mwakilishi wadi maalum Mary Mariach ambaye alisema kwamba hatua hiyo imechangia kukithiri utovu wa usalama mipakani pa kaunti hizi mbili kwani inakisiwa huenda bunduki zinazotumika katika uhalifu huu ni za maafisa hao.

Aidha Mariach alisema iwapo maafisa hao katika kaunti ya Pokot Magharibi hawatapewa silaha hizo basi zile ambazo zilitolewa kwa maafisa wa NPR kaunti ya Elgeyo marakwet zinapasa kutwaliwa ili kushuhudiwe amani.

“Tumeona kwamba bunduki za NPR ndizo zinatumika katika visa vingi vya utovu wa usalama kerio valley. Tunaomba serikali kwamba, iwapo maafisa wa NPR kutoka pande zote hawatapewa bunduki basi zile ambazo zilitolewa kwa wale wa Elgeyo marakwet zitwaliwe ndipo tuwe na amani.” Alisema Mariach.

Wakati uo huo Mariach alitoa wito kwa viongozi kutoka kaunti zote za bonde la Kerio kuketi chini na kubuni mikakati ambayo itahakikisha kwamba swala la utovu wa usalama katika kaunti hizi linapata suluhu ya kudumu kwani kwa sasa wengi wa wakazi katika kaunti hizi wanapitia hali ngumu.

“Kwa sasa watu wengi wanapitia hali ngumu ya maisha hasa njaa. Hivyo ombi langu kwa viongozi kutoka kaunti zote za bonde la kerio, ni waketi chini na kutafuta suluhu ya kudumu kwa swala hili la utovu wa usalama.” Alisema.