BARAZA LA WAZEE POKOT MAGHARIBI LAPEWA MAKATAA YA SIKU 21 KUFANYA UCHAGUZI MPYA.

Afisi ya mwanasheria mkuu wa serikali imelipa baraza la wazee katika kaunti ya Pokot magharibi siku 21 kufanya uchaguzi wa viongozi wake.

Kulingana na mshirikishi wa baraza hilo kanda ya kaskazini mwa bonde la ufa Wilson Lopeta, hatua hii imejiri kufuatia migawanyiko miongoni mwa wazee, makundi kadhaa yakiibuka na kupelekea kutokuwepo na umoja miongoni mwa wazee.

“Baraza la wazee liligawanyika katika makundi mbali mbali kutokana na malumbano ya kila mara. Hii ilisababishwa na miingilio ya kisiasa. Lakini sasa tumepokea barua kutoka kwa mwanasheria mkuu wa serikali ambapo tumepewa siku 21 kuhakikisha kwamba tunasuluhishwa swala hili na kufanya uchaguzi mpya.” Alisema Lopeta.

Naibu karani wa baraza hilo la wazee Josephat Tomee alisema migawanyiko miongoni mwa wazee imelemaza pakubwa shughuli ambazo wazee hao walikuwa wakitekeleza ikiwemo kuhakikisha amani inadumishwa miongoni mwa wakazi kanda hii.

“Hii itakuwa nafasi nzuri ya sisi kuendelea bila ya mivutano. Kwa sababu tuna shughuli nyingi ambazo zinapasa kufanywa na wazee ikiwemo maswala ya amani. Kama si kwa sababu ya migawanyiko hii, hatungekuwa na tatizo hili la usalama.” Alisema Tomee.

Kwa upande wake afisa katika shirika la kimataifa la Justice and Environment foundation Robert Kinywa ambaye aliandamana na wazee hao kutoa ushauri wa kisheria, alisema baraza hilo limekiuka sheria za katiba yake kwa kuhudumu miaka saba bila ya uchaguzi kwani kulifaa kuwa na uchaguzi wa viongozi wapya kila mwaka.

“Nimeangalia katiba yao na nimeona kwamba imeandikwa vizuri ila wale viongozi ambao wamekuwa afisini wamekwenda kinyume na sheria ya baraza hili. Sheria ya baraza hili inasema kwamba mtu anafaa kuwa afisini kwa mwaka mmoja ila hawa wamekaa afisini kwa miaka saba.” Alisema Kinywa.