OPARESHENI YA KIUSALAMA KASKAZINI MWA BONDE LA UFA YAENDELEA KUKOSOLEWA NA WADAU MAENEO HAYO.

Wanaharakati kaunti ya Pokot magharibi wamekosoa oparesheni ya kiusalama inayoendelezwa na maafisa wa polisi kwa ushirikiano na wale wa jeshi mipakani pa kaunti hiyo, kuwakabili wezi wa mifugo ambao wamekuwa wakiendeleza mauaji ya wakazi kando na kuiba mifugo.

Wakiongozwa na Sarich Joseph, wanaharakati hao wanadai kwamba oparesheni hiyo imekuwa ya kikatili kwa wakazi wa maeneo hayo ambapo badala ya maafisa wa usalama kuwalenga wahalifu, sasa wameanza kuwahangaisha wakazi.

Aidha Sarich alikosoa idadi ya maafisa wa usalama pamoja na silaha nzito ambazo zinatumika katika oparesheni hiyo

“Nashangaa sana kwamba watu wetu wa Pokot wamewekewa oparesheni. Wameleta maafisa wengi wa usalama ambao wanawahangaisha sana wakazi, wanawapiga watu, kina mama wanabakwa, watoto wanaumia, sasa tunashangaa sisi tuko nchi gani? Wamebeba silaha zote ambazo zinatumika kwa magaidi kama alshabaab kuendesha tu hii oparesheni.” Alisema Sarich.

Wakati uo huo Sarich alidai kwamba oparesheni hiyo inaendeshwa kwa ubaguzi ambapo jamii zingine zinapendelewa zaidi kuliko jamii ya kaunti hiyo, akitoa wito kwa rais William Ruto kuisitisha mara moja na kuangazia mbinu mbadala za kukabili visa vya ujangili maeneo hayo.

“Hii hali kwamba kuna watu wanapendelewa na wengine hawapendelewi katika oparesheni hii si nzuri. Sisi wote ni wakenya na tunafaa kushughulikiwa kwa usawa. Namwomba tu rais, tafadhali ,ondoa hii oparesheni na utumie njia nyingine ambayo itasaidia kuondoa uhalifu maeneo haya.” Alisema.