MAUAJI LAMI NYEUSI YAENDELEA KUSUTWA NA VIONGOZI POKOT MAGHARIBI.

Viongozi kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kushutumu mauaji ya watu watano eneo la Lami nyeusi mpakani pa kaunti hiyo na kaunti jirani ya Turkana ambapo pia mbuzi 18 waliibwa na wavamizi hao juma lililopita.

Akizungumza alipozuru eneo la tukio, mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto aidha alishutumu hali kwamba wavamizi hao wanaoaminika kutoka kaunti jirani walifanikiwa kutekeleza mauaji hayo hali kuna maafisa wa usalama ambao wanashika doria eneo hilo.

Wakati uo huo Moroto aliwalaumu baadhi ya viongozi wa kisiasa kwa matamshi ambayo wamekuwa wakiyatoa anayosema kwamba yanachochea kuendelea kushuhudiwa uvamizi huo.

“Tunaambiwa kwamba kuna doria za maafisa wa usalama eneo hili. Na doria bila matunda hazina maana yoyote. Tatizo ni viongozi wa kisiasa hasa wale wapya ambao wamechaguliwa mara ya kwanza mwezi agosti, wanarusha maneno kiholela ambayo yanachochea uhasama.” Alisema Moroto.

Moroto sasa anataka kuanzishwa miradi ya maendeleo maeneo hayo ili kukabili changamoto zinazoshuhudiwa na wakazi badala ya kuegemea tu oparesheni ya maafisa wa usalama ambayo bado haijazaa matunda tangu ilipoanzishwa.

“Tulitaka oparesheni ije huku ili maafisa wa jeshi wafungue miradi mbali mbali ya maendeleo jinsi ilivyokuwa enzi za rais muustaafu hayati Mwai Kibaki. Maeneo ya huku hayana maji na kwa upande mwingine raslimali zimechangia uhasama uliopo.” Alisema.