VIONGOZI BONDE LA KERIO WASUTA WIZARA YA USALAMA JINSI INAVYOSHUGHULIKIA UTOVU WA USALAMA ENEO HILO.
Naibu gavana kaunti ya Pokot magharibi Robert komole ameendelea kusisitiza haja ya serikali kupitia idara ya usalama kuangazia njia mbadala ya kukabiliana na utovu wa usalama eneo la bonde la kerio.
Akizungumza katika hafla Moja ya amani iliyowaleta pamoja viongozi wa kaunti hiyo na kaunti jirani ya Elgeyo marakwet, Komole alisema hatua ya kuwaajiri maafisa wa akiba NPR inazidisha uhasama miongoni mwa jamii zinazoishi eneo hili.
Badala yake Komole alipendekeza kutumika zaidi mikutano ya mashauriano baina ya viongozi wa kaunti husika pamoja na viongozi wa kidini ili kuafikiwa suluhu ya kudumu.
“Haya mambo ya kutumia maafisa wa NPR kudumisha usalama kerio valley ni kuzidisha tu uhasama. Kile tunahitaji ni kuongoza mikutano ya amani ikiongozwa na viongozi wa kidini na wanasiasa kutoka pandeo zote zinazozozana ili kupata suluhu ya kudumu.” Alisema Komole.
Kwa upande wake mwakilishi kina mama katika kaunti ya Elgeyo marakwet Carolyn Ngelechei alitishia kuwasilisha mswada bungeni wa kutaka kuwaondoa wakuu wa usalama afisini kwa kushindwa kudhibiti vitendo vya uhalifu bonde la kerio.
“Niliahidi na nitaendelea kuahidi kwamba tunapotarajiwa kurejelea vikao vya bunge, iwapo kutaendelea kushuhudiwa utovu wa usalama, nitawasilisha mswada bungeni wa kuwaondoa afisini wakuu wa usalama kwa kushindwa kudhibiti uvamizi kerio valley.” Alisema Ngelechei.