MADEREVA WASHUTUMU KAZI DUNI ILIYOTEKELEZWA KWENYE BARABARA YA KAPENGURIA –KACHELIBA.

Wahudumu wa magari kwenye barabara ya Kapenguria –Kacheliba hasa kutoka eneo la Kacheliba kaunti ya Pokot magharibi wameshutumu kile wamesema kwamba kazi duni iliyofanywa na mwanakandarasi aliyejenga barabara hiyo.

Wakiongozwa na Rashid Ebenyo wahudumu hao walisema kwamba barabara hiyo imeanza kuharibika chini ya mwaka mmoja tangu ilipojengwa, wakilalamikia pia kutowekwa ishara zozote za barabarani hali ambayo ni hatari kwa madereva na wahudumu wa boda boda.

“Tuliwekewa lami kwenye hii barabara ila sasa mashimo yamejaa chini ya mwaka mmoja tangu ijengwe. Hata ishara za barabarani pekee hamna. Matuta ambayo yaliwekwa ni machache sana ambapo ni hatari kwetu sisi.” Alisema Ebenyo.

Wahudumu hao sasa wanataka mwanakandarasi aliyejenga barabara hiyo kuwajibishwa na hata kuagizwa kuijenga upya na kuhakikisha kwamba ina ishara ili kuzuia ajali ambazo zimekuwa zikishuhudiwa mara kwa mara.

“Tunaomba hii barabara ibomolewe na ijengwe upya, waweke ishara za barabarani kwa sababu kumekuwa kukishuhudiwa ajali nyingi sana kwenye hii barabara kutokana na ukosefu wa ishara hizo.” Alisema.

Ni kauli ambayo ilisisitizwa na mwakilishi wadi maalum Bruno Lomenwa ambaye alisema kwamba licha ya mamilioni ya fedha za mlipa ushuru kutumika katika ujenzi wa barabara hiyo hali ni jinsi ilivyokuwa kabla ya kukarabatiwa akimtaka waziri wa barabara Kipchumba Murkomen kumchukulia hatua mwanakandarasi aliyepewa jukumu la kuishughulikia.

“Mwanakandarasi ambaye alipewa hii kazi alifanya kazi duni sana. Namwomba waziri wa barabara Kipchumba Murkomen kuzuru eneo hili na kushuhudia jinsi ilivyo barabara hii. Huyu mwanakandarasi anapasa kuchukuliwa hatua kwani mamilioni ya pesa ya walipa ushuru yalitumika kwa kazi hii duni.” Alisema Bruno.