WAHALIFU WAKAIDI OPARESHENI YA KIUSALAMA BONDE LA KERIO NA KUENDELEZA MASHAMBULIZI DHIDI YA RAIA.

Wahalifu wanaoendeleza  wizi wa mifugo wameendelea kutekeleza mashambulizi dhidi ya raia katika eneo la bonde la kerio licha ya oparesheni ya kiusalama ambayo inaendelezwa na maafisa wa polisi pamoja na kikosi cha jeshi la KDF eneo hilo.

Hii ni baada ya watu wawili ikiwemo mwanafunzi wa gredi ya saba kuripotiwa kuuliwa na wahalifu hao katika visa viwili tofauti alhamisi eneo la Chesogon mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo marakwet.

Katika kisa cha kwanza inaarifiwa kwamba mkazi mmoja wa elgeyo marakwet aliuliwa baada ya kusikika milio ya risasi eneo hilo, na baada ya masaa machache mwanafunzi wa gredi ya saba akauliwa eneo la Cheptulel katika kisa kinachaminika kuwa cha kulipiza kisasi.

“Risasi zilisikikika kwenye mpaka wa Pokot na marakwet ambapo mkazi mmoja wa marakwet aliuliwa, hadi barabara huku zikafungwa kufuatia ukosefu wa usalama. Baadaye kufikia mwendo wa saa kumi mtoto wa gredi ya saba akapigwa risasi na wamarakwet ambao wamekuwa wamejificha kando ya barabara kulipiza kisasi kwa kuuliwa mmarakwet.” Alisema mkazi mmoja.

Inaarifiwa mwanafunzi huyo na wenzake wawili walikuwa katika harakati zao baada ya kurejea nyumbani kwa likizo fupi iliyoanza alhamisi kabla ya kukutana na mauti ambapo wengine wawili walinusurika baada yao kutorokea usalama wao.

“Hawa watoto walikuwa watatu wakitembea barabarani baada ya kurudi kwa likizo fupi. Sasa wawili kati yao walitoroka waliposikia risasi zikilia. Ila huyo mmoja alipigwa risasi akaaga dunia.” Alisema.