SERIKALI YAWAHAKIKISHIA WAKAZI SULUHU KWA TATIZO LA MAJI POKOT MAGHARIBI.
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi imeendelea kuweka mikakati ya kukabili tatizo la uhaba wa maji ambalo limekumba jamii nyingi maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo na ambao umechangiwa pakubwa na hali ya ukame unaoshuhudiwa.
Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na kituo hiki, waziri wa maji na mazingira Lucky Litole alisema kwamba serikali kupitia wizara yake inaendeleza shughuli ya kuchimba visima maeneo ambayo yameathiriwa pakubwa na uhaba wa bidhaa hiyo muhimu.
Alisema wanapanga kuchimba visima 21 katika kaunti hiyo ambapo kufikia sasa visima 13 tayari vimechimbwa, saba miongoni mwavyo vikiwa tayari vimekamilika vikisubiriwa kuanza kuhudumu ili wakazi wa maeneo husika waanze kupata maji safi ya matumizi.
Aidha Litole alisema visima zaidi vitachimbwa katika kipindi kijacho cha matumizi ya fedha za serikali.
“Tuna mipango ya kuchimba visima 21 kaunti nzima. Kwa sasa tumefikisha visima 13 ambapo miongoni mwa hivyo ni saba ambavyo viko tayari kutumika. Tunatarajiwa kuchimba visima zaidi katika kipindi kijacho cha matumizi ya fedha za serikali.” Alisema Litole.
Wakati uo huo Litole alitoa wito kwa wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi kuwa na mazoea ya kupanda miti na kutunza misitu ili kukabili mabadiliko ya tabia nchi hatua aliyosema kwamba italeta suluhu kwa tatizo la ukame ambao umekuwa ukishuhudiwa mara kwa mara kaunti hiyo.
“Tukiweza kupanda miti itatusaidia kuwa na mvua kwa muda mrefu na pia kuzuia maporomoko ya udongo.Nawaambia wananchi kwamba ni jukumu letu kuhakikisha kwamba misitu inatunzwa kwani ndio suluhu ya pekee kwa mabadiliko ya tabia nchi.” Alisema.