MASOMO KATIKA SHULE ZA JUNIOR SECONDARY YAKABILIWA NA CHANGAMOTO.
Wadau katika sekta ya elimu kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kulalamikia changamoto ambazo zinakabili utekelezwaji wa mtaala mpya wa elimu CBC.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya St Brendan Chelomoi Julius Murei alisema kwamba licha ya kuanza masomo ya shule ya sekondari ya msingi katika shule hiyo wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vitabu hali inayofanya vigumu kuendeleza masomo hayo.
Aidha murei alilalamikia uhaba wa walimu wa kuwafunza wanafunzi wa gredi ya saba pamoja na fedha zilizoahidiwa na serikali kufanikisha elimu ya shule ya sekondari ya msingi.
“Kufikia sasa tumeanza masomo ya junior secondary lakini bado tuna changamoto nyingi sana. Kwanza kabisa hatuna walimu wa kutosha, hatuna vitabu vya kutekeleza masomo hayo na pia hatujapata pesa kutoka kwa serikali kwa hivyo imekuwa vigumu kuwashughulikia watoto hawa.” Alisema Murei.
Murei alitoa wito kwa serikali kuhakikisha kwamba inaharakisha kutimiza ahadi ilizotoa za kutoa raslimali za kufanikisha masomo hayo ya shule za sekondari ya msingi ili kuwawezesha wanafunzi hao kuendelea na masomo yao bila ya changamoto.
“Tunaomba serikali kuhakikisha kwamba inatimiza ahadi zake na kuwasilisha mahitaji ya kufanikisha elimu hii ya CBC hasa kwa wanafunzi wa shule za junior secondary.” Alisema.