WADAU WA ELIMU WAANDAA KIKAO CHA KUTATUA MZOZO UNAOKUMBA SHULE YA KAMOTING POKOT MAGHARIBI.
Mkurugenzi wa elimu kaunti ndogo ya Kapenguria katika kaunti ya Pokot magharibi Amos Kibet amewalaumu wazazi wa shule ya msingi ya Kamoting kuhusiana na jinsi ambavyo wameshughulikia lalama ambazo wamekuwa nazo kuhusiana na uongozi wa shule hiyo.
Akizungumza katika kikao na wazazi hao ambao walimfurusha mwalimu mkuu wa shule hiyo, Kibet alisema kwamba kuna taratibu ambazo zinapasa kufuatwa katika kulalamikia uongozi wa shule yoyote badala ya kuchukua sheria mikononi.
Aidha Kibet aliwalaumu wazazi wa shule hiyo kwa kusalia kimya wakati uongozi wa shule hiyo unakiuka maagizo ya serikali kwa kuwatoza fedha kabla ya kutoa huduma kwa wanafunzi.
“Yalikuwa makosa makubwa kwa wazazi kuvamia shule na kumfurusha mwalimu mkuu. Kuna njia za kusuluhisha mizozo ambayo inakumba shule. Inanishangaza kuona kuwa mmenyamazia haya mambo yote ambayo yamekuwa yakiendelea kwa hii shule. Haya maswala ya kuitisha pesa kiholela kutoka kwa wazazi hayaruhusiwi.” Alisema Kibet.
Ni kauli ambayo ilisisitizwa na naibu mkurugenzi wa tume ya huduma kwa walimu TSC kaunti hiyo Jane Nyaoke ambaye aidha alisema kwamba ni jukumu la jamii kuhakikisha usalama wa walimu.
“Sisi kama TSC hatutumi walimu shuleni kuchapwa, na ndiyo maana kilipofanyika kitendo hicho tuliwaambia walimu kutafuta sehemu watakuwa salama na ndiyo maana walilazimika kuondoka kwa muda. Lakini ni jukumu la jamii kuhakikisha usalama wa walimu kwa sababu kazi yao ni kufunza watoto.” Alisema Nyaoke.
Kwa upande wake mwakilishi wadi ya Mnagei Richard Todosia alitoa wito kwa serikali kuendesha elimu ya kuwafahamisha wazazi kuhusu elimu ya shule za sekondari ya msingi ili kuzuia hali ambapo baadhi ya watu wanatumia fursa ya mkanganyiko uliopo kuhusu shule hizo kuwapunja wazazi.
“Serikali inapasa kuendesha elimu kwa wazazi kuhusu elimu ya shule za junior Secondary ili kuzuia hali ambapo baadhi ya watu wanatumia kutokuwa na ufahamu kwa wazazi kuhusu zinavyoendeshwa shule hizo kuwapunja.” Alisema Todosia.
Wazazi wa shule hiyo walielezea kuridhishwa na hatua ambazo zimepigwa katika kikao hicho wakielezea imani ya kurejelewa shughuli za masomo japo wakisisitiza kupewa uhamisho mwalimu mkuu wa shule hiyo.