MACHIFU SIGOR WATAKA MBINU YA KUTWAA SILAHA KUTOKA MIKONONI MWA WAKAZI KUBADILISHWA.

Machifu wa eneo bunge la sigor katika kaunti ya Pokot magharibi wametoa wito wa kubadilishwa mbinu za kuendesha oparesheni ya kutwaa silaha haramu ambazo zinamilikiwa na raia eneo hilo.

Wakiongozwa na chifu wa eneo la Songop Joseph Korkimul, machifu hao walisema kwamba serikali ingetumia mbinu ya kuhubiri amani miongoni mwa wakazi kabla ya kuwataka kusalimisha silaha hizo hatua waliyosema kwamba ingezaa matunda ikilinganishwa na mbinu inayotumika kwa sasa.

Walisema kwamba kutwaa silaha hizo kwa lazima kunawafanya wengi wao kuona serikali na wakuu wa usalama kuwa maadui hatua ambayo huenda ikafanya vigumu kwao kuzisalimisha.

“Ingefaa mwanzo tuhubiri amani ili watu wakishatulia na ndipo tawahimize walete bunduki haramu, hiyo itakuwa rahisi. Lakini sasa wakati ambapo kuna mavamizi ya hapa na pale itakuwa vigumu kwa sababu sasa wataona maafisa wa usalama kuwa maadui na inafanya vigumu kwao kusalimisha silaha hizo.” Alisema Korkimul.

Kauli ya machifu hao inajiri wakati wakazi wa eneo hilo hasa wafanyibiashara wakilalamikia amri ya kutotoka nje wakisema kwamba amri hiyo imeathiri pakubwa shughuli zao za kila siku ikizingatiwa hali ngumu ya uchumi sasa.

“Hii curfew ambayo inaendelezwa inatuathiri sana kwa sababu wakati ambapo tunafaa kufanya sasa shughuli zetu za kibiashara vizuri ndio wakati tunafukuzwa na polisi. Kwa hivyo tunasema oparesheni hii ipelekewe maeneo ambako kuna wahalifu. Sisi huku hata hatujawahi kuona bunduki, na tunashangaa oparesjheni hii inafanywa huku ni ya nini?” Walilalama wakazi.