KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI YAPOKEA DAWA ZA KIMA CHA SHILINGI MILIONI 43 KUTOKA KEMSA.


Shirika la kusambaza dawa na vifaa vya matibabu KEMSA limeipokeza kaunti ya Pokot magharibi dawa za kima cha shilingi milioni 43 huku likiahidi kusambaza kiwango kilichosalia kabla ya mwisho wa juma hili.
Akizungumza wakati akipokea dawa hizo gavana Simon Kachapin alilipongeza shirika hilo ambalo alisema kwamba limeimarisha huduma zake hasa kuhusu usambazaji wa dawa kwa kaunti kwa wakati, huku akiwataka wahudumu wa afya katika vituo mbali mbali vya afya kutumia vyema dawa hizo.
“Nataka kushukuru KEMSA kwa sababu ya marekebisho ambayo yametekelezwa kwenye shirika hilo ambayo yameimarisha huduma. Sasa tunapokea dawa kwa wakati.” Alisema.
Kachapin aliongeza kwa kusema, “ Pia natumia fursa hii kuwahimiza wahudumu wa afya kaunti hii kuhakikisha kwamba wanatumia vyema dawa hizi. Hatutaki kusikia kwamba dawa zimeibwa kwa sababu ni laana kubwa sana kuiba dawa ambazzo zinakusudiwa kuwasaidia wagonjwa.”
Ni kauli ambayo ilitiliwa mkazo na waziri wa afya kaunti hiyo Cleah Parklea ambaye aidha alisema kwamba dawa hizo zimeigharimu pakubwa serikali ya kaunti na yatakuwa makosa makubwa iwapo zitakosa kufanya kazi iliyokusudiwa kwa kuporwa na watu wachache.
“Serikali ya kaunti hii imetumia pesa nyingi sana kununua dawa hizi na haitakuwa habari nzuri kusikia kwamba kuna watu ambao wanaiba dawa. Tuzitumie vizuri ili wagonjwa wapate huduma inayostahili.” Alisema Parklea.
Kwa upande wake mwakilishi wa shirika hilo kanda ya kaskazini mwa bonde la ufa Zaccheus Muya aliipongeza kaunti ya Pokot magharibi kwa ushirikiano ambao inalipa shirika hilo kupitia kwa kulipa madeni yake akisema kuwa katika kanda hii ni kaunti hiyo pekee ambayo haina deni la KEMSA.
“Katika eneo hili ni kaunti ya Pokot magharibi pekee ambayo haina deni na shirika la KEMSA. Naipongeza sana kaunti hii kwa ushirikiano ambao imeonyesha kwa shirika la KEMSA.” Alisema Muya.