WAAKILISHI WADI POKOT MAGHARIBI WAKOSOA OPARESHENI YA KIUSALAMA.


Waakilishi wadi katika kaunti ya Pokot magharibi wamelalamikia jinsi serikali inavyoshughulikia swala la utovu wa usalama katika kaunti za bonde la Kerio, wakisema kwamba ipo njia bora na salama inayoweza kutumika bila kuwahangaisha wakazi kupitia oparesheni za maafisa wa polisi.
Katika kikao na wanahabari viongozi hao wakiongozwa na kiongozi wa walio wengi katika bunge la kaunti hiyo Martine Komongiro, walisema kwamba wakuu wa usalama wanafaa kuandaa kikao na viongozi kutoka kaunti zinazoshuhudia utovu wa usalama ili kubaini chanzo cha tatizo hili.
“Serikali inapasa kuketi chini na viongozi wa maeneo ambayo kuna tatizo la usalama na kujadiliana nao ili kufahamu tatizo liko wapi. Baada ya kufahamu chanzo cha utovu wa usalama itakuwa rahisi kutafuta suluhu na haitakuwa lazima kuendeleza oparesheni za kiusalama.” Walisema viongozi hao.
Viongozi hao aidha waliikosoa serikali kwa kuibagua kaunti hiyo katika mchakato mzima wa kutafuta amani eneo la bonde la kerio, wakidai kwamba kaunti zingine zimekuwa zikipendelewa zaidi huku wakazi wa kaunti ya Pokot Magharibi wakilaumiwa kuwa chanzo cha utovu wa usalama.
“Waziri wa usalama alitembelea Baringo, Turkana na Elgeyo marakwet ila hajawahi kukanyaga kaunti hii ya Pokot magharibi. Tunamweleza waziri huyo kwamba anapokuja kusikiliza maoni ya wakazi kuhusiana na hali hii atembelee pande zote husika ila si kufanya mambo kwa kuwabagua watu wengine na kisha tunaanza kulaumiwa kwamba wapokot ndio wabaya.” Walisema.
Walisema hatua ya kukamatwa viongozi wa kaunti hiyo kwa madai ya kuchochea utovu wa usalama haitasaidia kwa vyovyote bali itachochea hata zaidi ghadhabu za wakazi, wakisema badala yake serikali inapasa kuangazia maendeleo maeneo haya na kuhakikisha elimu inapewa kipau mbele miongoni mwa wakazi.
“Hili swala la kukamatwa viongozi wa kaunti hii kuwa ndio wanaochochea utovu wa usalama halitasaidia bali ndio mwanzo litazidisha hasira kwa wananchi. Serikali inafaa kuangazia maendeleo maeneo haya na kuhakikisha kwamba kila mtoto anapata elimu ndipo hali hii itapata suluhu.” Walisema.