WAKAZI MASOL WALALAMIKA KUATHIRIKA NA AMRI YA KUTOKUWA NJE.
Aliyekuwa mwakilishi wadi ya Masol eneo bunge la Sigor katika kaunti ya Pokot magharibi Ariong’o Loporna amelalamikia utekelezwaji wa amri ya kutokuwa nje kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa kumi na mbili asubuhi.
Akizungumza na wanahabari Loporna alitaka muda wa kutekelezwa amri hiyo kupunguzwa akisema kwamba ikiendelea kutekelezwa jinsi ilivyo, itaathiri pakubwa shughuli za wakazi wa eneo hilo anaosema kwamba wengi wao huanza shughuli zao nyakati za alfajiri hasa ikizingatiwa hali ngumu ya kiuchumi kwa sasa.
“Upande wa huku watu ni wakulima. Na kwa sababu hiyo, wao huuza bidhaa zao hadi majira ya saa tatu usiku ndipo wanaelekea nyumbani. Na wengine huamka mapema kulingana na shughuli zao lakini sasa tunaona mambo haya ya curfew yataathiri zaidi watu wengi.” Alisema Loporna.
Ni kauli ambayo ilikaririwa na wahudumu wa boda boda eneo hilo ambao kupitia mwenyekiti wao Joseph Toitoi walisema kwamba shughuli zao za kila siku zimeathirika pakubwa kwani wao hufanya shughuli zao nyakati za alfajiri na jioni kufuatia makali ya jua nyakati za mchana.
“Sisi kama wahudumu wa boda boda tumeathirika zaidi kwa sababu kazi yetu huanza saa kumi na mbili asubuhi na ikifika saa nne tunaanza kuweka kwenye kivuli pikipiki zetu hadi saa kumi na mbili jioni kutokana na joto kali la eneo hili. Sasa tangu curfew kuanza tumekuwa tukirejea nyumbani bila chochote.” Alisema Toitoi.
Hata hivyo naibu kamishina eneo la Pokot ya kati Jeremiah Koech Tumo aliwataka wakazi wa eneo hilo kushirikiana na maafisa wa usalama katika shughuli nzima akisema kwamba ni kwa manufaa ya mwananchi wa kawaida ili maisha yarejelee hali ya kawaida.
“Hii oparesheni inaendeshwa kwa manufaa ya jamii katika kaunti husika. Kile tunaomba ni kwa wananchi kushirikiana na maafisa wa polisi kuhakikisha kwamba oparesheni hii inafaulu ili maisha yarejee katika hali yake ya kawaida.” Alisema Tum.