WADAU WAENDELEZA MIKAKATI YA KUKABILI ATHARI ZA UKAME POKOT MAGHARIBI.


Maeneo ya pokot ya kati na pokot kaskazini katika kaunti hii ya Pokot magharibi ndiyo yaliyoathirika zaidi na hali ya ukame ambayo imeendelea kushuhudiwa nchini.
Haya yalibainika katika kikao cha wadau mbali mbali hasa kutoka idara za serikali kuhusiana na mikakati iliyopo na hatua ambazo zitachukuliwa kushughulikia hali hii mkurugenzi wa idara ya kukabili majanga kaunti hiyo NDMA Joshua Mayeku akisema hali hii imetokana na kufeli kwa mvua ya vuli iliyosubiriwa mwaka jana.
“Kulikuwa na dalili kwamba mambo si kawaida mwaka uliopita kwa kuwa kulikuwa na msimu wa mvua za vuli ambayo ilikuwa chini sana ya kiwango kilichotarajiwa. Kaunti ndogo mbili zimeathirika zaidi kutokana na ukame ikiwa ni pamoja na pokot ya kati na pokot kaskazini.” Alisema Mayeku.
Mkurugenzi wa idara ya hali ya anga katika kaunti hii Wilson Lonyang’ole alielezea haja ya wakulima kuangazia mbinu tofauti ya shughuli zao za kilimo ikiwa ni pamoja na kupanda mimea ya nyakati za zamani na kutotegemea tu ufugaji kama njia moja ya kukabili athari za mabadiliko ya anga.
“Tunawashauri wananchi kutotegemea kilimo cha ufugaji pekee bali wakumbatie hata kilimo cha upanzi wa mimea hasa ile ya zamani kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.” Alisema Lonyang’ole.
Kwa upande wake naibu mkurugenzi wa idara ya mazingira Raphael Magal alipongeza serikali ya kaunti kwa kushirikiana na wadau hao hasa katika kubuni kamati zitakazoshughulikia maswala ya mazingira katika kaunti hii.
“Naishukuru serikali ya kaunti kwa ushirikiano ambao imetupa kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi kwa vile imetusaidia kubuni kamati ambazo zitashughulikia maswala ya mazingira katika kaunti hii yetu.” Alisema Magal.