IDARA YA TRAFIKI POKOT MAGHARIBI YAENDELEZA MIKAKATI YA KULETA NIDHAMU KATIKA SEKTA YA BODA BODA.


Wahudumu wa boda boda mjini Kapenguria katika kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kuzingatia kikamilifu sheria za barabarani ili kuhakikisha kwamba nidhamu inadumishwa na kuzuia ajali za mara kwa mara.
Akizungumza wakati wa kuhamasisha wahudumu hao kuhusiana na sheria za barabarani, kamanda wa trafiki kaunti hiyo Catherine Wanyika amewataka wahudumu hao kutobeba zaidi ya abiria wawili kwenye pikipiki, kuhakikisha wanavalia magwanda rasmi pamoja na kuripoti panapotokea ajali na kutochukua sheria mikononi mwao.
“Tumeanzisha uhamasisho huu kwa wahudumu wa boda boda ili kuwafunza kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria za barabarani, ikiwemo kubeba idadi hitajika ya abiria ambao ni wawili kwa kila pikipiki, kuvalia magwanda rasmi na pia kuwa na mazoea ya kuripoti panapotokea ajali na kutochukua sheria mikononi.” Alisema Wanyika.
Wanyika alisema kwamba wataendeleza uhamasisho huo sehemu tofauti za kaunti hiyo katika juhudi za kuhakikisha kwamba wahudumu hao wanafahamu vyema sheria za barabarani na kuzuia ajali pamoja na kukabiliana na visa vya wizi ambavyo mara nyingi huhusishwa na sekta hiyo.
“Ajali pamoja na wizi unaohusiana na boda boda umekithiri katika siku za hivi karibu na hivyo tumeamua kuwahamasisha wahudumu hawa maeneo mbali mbali ya kaunti hii kama njia moja ya kuhakikisha nidhamu katika sekta hiyo.” Alisema.
Ni hatua ambayo ilipongezwa na wahudumu hao kupitia mwenyekiti wao Laban Ruto wakisema kuwa mafunzo hayo yameangazia pakubwa changamoto ambazo wamekuwa wakikumbana nazo katika shughuli zao za kila siku wakitoa wito wa kuimarishwa usalama wao.
“Tunashukuru sana kwa mafunzo haya maana yamegusia pakubwa changamoto ambazo zinatukumba kwenye sekta hii, ikiwemoa ajali za kila mara pamoja na utovu wa usalama ambapo pikipiki za watu wengi zimekuwa zikiibwa. Tunachoomba tu ni kwa serikali kuimarisha usalama wetu tunapotekeleza shughuli zetu za kila siku.” Alisema Ruto.