SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAENDELEA KUWEKA MIKAKATI YA KUHAKIKISHA USALAMA UNADUMISHWA.
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi imefungua barabara ya kutoka karawal kuelekea Kapushen hadi Kongolokwan mpakani pa maeneo bunge ya pokot kusini na Sigor kama baadhi ya juhudi za kuimarisha usalama maeneo hayo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa barabara hiyo waziri wa barabara katika kaunti hiyo Joshua Ruto alisema kwamba kando na kuhakikisha usalama unaimarishwa hasa baina ya jamii za pokot na marakwet, barabara hiyo pia itaboresha uchumi wa eneo hilo kwa kuwawezesha wakazi kusafirisha bidhaa zao sokoni.
“Barabara hii itaunganisha jamii ya Pokot na marakwet katika mlima wa Kamalogon. Licha ya kwamba ni barabara ya kiusalama itaboresha pia uchumi wa eneo hili kwa kuwawezesha wakulima kusafirisha bidhaa zao hadi sokoni bila tatizo.” Alisema Ruto.
Ni kauli ambayo ilikaririwa na mwakilishi wadi ya Tapach Samwel Korinyang ambaye aidha alisema wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakihangaika katika kupata huduma muhimu za serikali kutokana na ukosefu wa barabara.
“Barabara hii itafungua eneo hili na kuwawezesha wakulima kufikisha bidhaa zao sokoni. Watu wanalima viazi huku kwa wingi ila havifiki sokoni kutokana na ukosefu wa barabara. Pia itahakikisha kwamba wakazi wanapata huduma muhimu za serikali.” Alisema Korinyang.
Wakazi wa eneo hilo walipongeza hatua hiyo wakisema kwamba itasaidia pakubwa katika kuimarisha hali ya usalama kwa kuwawezesha maafisa wa usalama kupiga doria bila ya kuwa na vikwazo vya kushindwa kupenya baadhi ya maeneo.
“Tunaipongeza sana serikali kwa barabara hii kwa sababu itasaidia sana eneo hili kuwa na amani kwa kuwawezesha maafisa wa usalama kupiga doria kila sehemu ya eneo hili bila kikwazo.” Walisema.