RAIS RUTO ATAKIWA KUFANYA KILA JUHUDI KUMALIZA UHALIFU ULIOKITHIRI BONDE LA KERIO

.
Viongozi mbali mbali kutoka eneo la bonde la kerio sasa wanamtaka rais William Ruto kufanya kila awezalo kuhakikisha kwamba usalama umerejeshwa eneo hilo na kukomesha mahangaiko ya wakazi kwenye maeneo husika.
Wakizungumzia mauaji ya maafisa wa usalama eneo la Kainuk mpakani pa kaunti hii ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana, viongozi hao wakiongozwa na seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandagor walisema ni wakati rais Ruto anafaa kufanya juhudi zote kukomesha uhalifu huo katika kaunti za Pokot magharibi, Baringo Turkana Elgeyo marakwet na maeneo mengine.
“Janga lilitokea eneo la Kainuk ambapo tulipoteza maafisa wa usalama. Tunamwomba rais kuwasaidia hao maafisa walio eneo hilo na ndege ili waweze kupamba na hao majangili.” Alisema Mandagor.
Naye rais Ruto alisema atafanya kila awezalo na kwamba amemwagiza waziri wa usalama wa kitaifa Prof. Kithure Kindiki kuhakikisha anafanya mipango ya kuhakikisha usalama unarejeshwa maeneo hayo na kukomesha mauaji ya maafisa wa usalama na wakazi wa eneo hilo kiholela.
Rais alisema ana mipango mahususi kuhakikisha kuna usalama na wanaoendeleza uhuni huo wanaweza kukabiliwa na mkono wa sheria.
“Nimemwambia waziri wa usalama Prof. Kithure Kindiki atoke katika afisi ya Nairobi, aende aishi eneo la kaskazini mwa bonde la ufa hadi hili swala la wananchi kupoteza maisha yao liishe. Tumeweka mipango kabambe na kupitia uwezo wote wa serikali tutahakikisha wajeuri hao wanakabiliwa vilivyo.” Alisema rais Ruto.
Kauli hizi zilijiri baada ya polisi katika kituo cha Kainuk mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana kupata miili mitatu ya maafisa wanne wa polisi waliotoweka wawili kati yao wakiwa maafisa wa kitengo cha GSU.
Kulingana na taarifa ya idara ya polisi, maafisa hao kutoka kituo hicho cha kainuk walikuwa wametembelea eneo ambako wahalifu walivamia gari la abiria usiku wa alhamisi katika barabara ya kitale-Lodwar takriban kilomita 5 kutoka kambi ya shirika la wanyamapori KWS, kuchunguza kisa hicho kabla ya kukumbana na miili ya tatu hao.
Maafisa waliouliwa walipatikana wakiwa uchi wa mnyama ambapo inaaminika wahalifu waliotekeleza mauaji hayo walitoweka na sare zao pamoja na bunduki walizokuwa nazo.
Magari yaliyokuwa yakitumika na maafisa hao pia yalitekeletezwa na wahalifu.