VISA VYA WATAHINIWA WA KCPE AMBAO HUENDA WAKAKOSA KUJIUNGA NA KIDATO CHA KWANZA KUFUATIA KARO VYAZIDI KURIPOTIWA.
Wanafunzi waliofanya mtihani wa KCPE mwaka 2022 wakiendelea kuripoti katika shule mbali mbali za upili walizoitwa idadi ya wanafunzi wanaohitaji ufadhili wa kuendeleza elimu yao ya shule ya upili imeendelea kuongezeka nchini licha kufanya vyema katika mtihani wao wa kitaifa.
Dorcas Ikanya ni mwanafunzi aliyesomea shule ya msingi ya wasichana ya Kacheliba ambaye alipata alama 280 na ambaye ameelezea hofu ya kukatiza ndoto yake baada ya maombi yake ya kutaka ufadhili kutoka mashirika mbali mbali kukataliwa.
Ametoa wito kwa wafadhili kujitokeza kumsaidia kutokana na hali duni ya kifedha ya familia baada ya babake kutoweka nyumbani miaka mingi iliyopita.
“Nimetuma maombi kwa mashirika yanayofadhili elimu kwa wanafunzi kutoka jamii masikini kama vile benki ya Equity lakini si kupata. Na sasa nipo nyumbani na nahofia nisipoenda shule maisha yangu yataathirika hali kuna wangine wanaonitegemea. Naomba wahisani kunisaidia niende shule.” Alisema Dorcas.
Aidha Joy Neema aliyepata alama ya 292 pia anakabiliwa na tishio la kukatiza ndoto yake baada ya kukosa namna ya kujiunga na kidato cha kwanza kutokana na ukosefu wa fedha hali iliyomlazimu kutoweka nyumbani kwenda kuomba nafasi katika shule moja ya upili.
“Nilipata alama 292 ila sina jinsi ya kujiunga na kidato cha kwanza. Mamangu anafanya tu kazi za vibarua ili tupate chakula na sasa sina wa kunilipia karo shuleni.” Alisema Joy.
Kulingana na mamake Joy Judith Andia, mmewe alitoweka nyumbani baada kutangazwa matokeo ya mtihani wa kitaifa kwa darasa la nane KCPE na sasa hana namna ya kugharamia elimu ya mwanaye akielezea hofu ya mwanawe kuathiriwa pakubwa na mazingira anamokaa iwapo hatapata msaada.
“Msichana wangu alitoweka nyumbani siku tatu zilizopita na nimekuwa nikimfuatilia ambapo nimempata shule ya Bakhita akiomba nafasi ya kuingia shuleni. Babake alitoweka punde matokeo ya mtihani yalipotangazwa. Naomba wahisani wanisadie mwanangu asome.” Alisema Andia.