WAKAZI POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUTOTEGEMEA KILIMO CHA MIFUGO NA BADALA YAKE KUANGAZIA KILIMO MBADALA.


Wito umetolewa kwa wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi kuendelea kusalia watulivu serikali inapoendeleza mikakati ya kuhakikisha kwamba wanapokea mbolea ya ruzuku baada ya kukamilika zoezi la kuwasajili wakulima watakaopokea mbolea hiyo.
Naibu kamishina wa eneo la pokot kaskazini James Ajwang alisema kwamba mbolea hiyo itaanza kusambazwa mara tu itakapopokelewa, akielezea imani kwamba wakulima watakuwa katika nafasi bora ya kuendeleza kilimo kufuatia mbolea hiyo ya bei nafuu na hivyo kukabili tatizo la njaa.
“Tumesajili wakulima na kilichosalia sasa ni serikali kuwasilisha mbolea ambayo itapiga jeki shughuli za kilimo katika kaunti hii ya Pokot magharibi. Nawasihi wakulima kusalia watulivu tunaposubiri serikali kuleta mbolea hiyo.” Alisema Ajwang.
Ajwang alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakazi kutotegemea zaidi kilimo cha ufugaji na badala yake kuangazia kilimo mbadala hasa cha upanzi wa mimea ili kuhakikisha kwamba wanakuwa na chakula cha kutosha kitakachowasaidia hata nyakati za kiangazi.
“Naihimiza jamii ya kaunti hii kuzingatia kilimo mbadala hasa kilimo cha mimea na kutotegemea tu mifugo kwa sababu sasa inakuwa vigumu kutegemea ufugaji kutokana na kiangazi cha muda mrefu kinachotokana na mabadiliko ya hali ya anga.” Alisema.
Hata hivyo aliahidi kwamba licha ya hali ya sasa ambapo idadi kubwa ya wakazi wa kaunti hiyo wanakabiliwa na makali ya njaa serikali itahakikisha kwamba hamna mkazi hata mmoja atakayepoteza maisha kutokana na ukosefu wa chakula.
“Tuna tatizo kubwa la baa la njaa. Idadi kubwa ya wakazi hapa wanategemea chakula cha msaada. Kama serikali tutahakikisha kwamba hamna mtu anayefariki kutokana na makali ya njaa.” Alisema.

WhatsApp us