WAHISANI WAOMBWA KUWASAIDIA WAKAZI WANAOKABILIWA NA BAA LA NJAA POKOT MAGHARIBI.


Mbunge wa kacheliba kaunti ya Pokot magharibi Titus Lotee ametoa wito kwa wahisani wakiwemo mashirika yasiyo ya serikali kujitokeza na kuwasaidai wakazi wa kaunti hiyo ambao wanakabiliwa na baa la njaa.
Lotee alisema kwamba hali ya ukame imekithiri katika maeneo mengi ya kaunti ya Pokot magharibi huku idadi ya wakazi wanaohitaji chakula ikiongezeka zaidi akisema kwamba chakula ambacho kimetolewa na serikali hakitoshelezi mahitaji ya waathiriwa.
Alisema eneo hilo halijapokea mvua ya kutosha kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita hali ambayo imeathiri pakubwa shughuli za kilimo kwa wakazi.
“Tunashukuru kwa kile ambacho serikali kuu na ya kaunti zimeleta kwa ajili ya watu wetu wanaokabiliwa na baa la njaa. Lakini ningependa kuomba jamii na mashirika yasiyo ya serikali pamoja na wahisani wengine watusaidie kwa sababu eneo hili halijapokea mvua ya kutosha kwa kipindi cha miaka tano iliyopita.” Alisema Lotee.
Wakati uo huo Lotee aliitaka serikali kushughulikia tatizo la maji hasa eneo la Pokot kaskazini ambako alisema wakazi wanalazimika kwenda muda mrefu kutafuta maji hali anayosema kwamba ni moja ya vyanzo vya utovu wa usalama kwenye baadhi ya maeneo ya kaunti hiyo.
“Hatuna maji kabisa. Watu wanalazimika kutembea kilomita nyingi kutafuta maji. Naomba serikali kuu pamoja na mashirika ya maji watutafutie maji kwa sababu uhaba wa maji ni moja ya vyanzo vya utovu wa usalama maeneo mengi ya kanda hii.” Alisema.