VIONGOZI WASHINIKIZA KUBADILI MBINU ZINAZOTUMIKA KUKABILI WIZI WA MIFUGO BONDE LA KERIO.


Viongozi wa kaunti ya Pokot magharibi kwa ushirikiano na idara za usalama waliendeleza mikutano ya amani maeneo ya mipakani pa kaunti hiyo na kaunti jirani ambako kumekuwa kukishuhudiwa visa vya utovu wa usalama katika juhudi za kusaka amani maeneo hayo.
Viongozi hao walielekeza jumanne mikutano hiyo eneo la Ompolion, ambako mbunge wa Sigor Peter Lochakapong alisema huenda tatizo la utovu wa usalama limesalia changamoto maeneo haya kutokana na mbinu ambazo zinatumika na maafisa wa usalama kukabili visa hivyo wakitaka mbinu hizo kubadilishwa.
“Kila kona sasa maeneo haya imekosa usalama na huenda mbinu ambazo zinatumika na serikali kukabiliana na hali hii haziwezi kusaidia kwa sasa. Maafisa wa usalama wanapasa kubadilisha mbinu za kukabili hali hii.” Alisema Lochakapong.
Viongozi hao pia walitumia mikutano hiyo kuendeleza shutuma kwa maafisa wa polisi waliowapiga risasi na kuwauwa zaidi ya Ng’ombe 100 eneo la Kainuk wakishinikiza hatua kuchukuliwa dhidi ya poilisi waliohusika ukatili huo.
“Nimetumikia serikali nyingi ila sijawahi kuwaona maafisa wa polisi wanaamka na kuanza kuwafyatulia risasi ng’ombe. Hao polisi waliohusika ukatili huo wanapasa kukamatwa na kuchukuliwa hatua kwa hasara ambayo wamesababishia wananchi.” Alisema mbunge wa kapenguria Samwel Moroto.
Naibu kamishina wa pokot kaskazini james Ajwang alipendekeza kujengwa kituo cha polisi eneo hilo la Ompolion kuhakikisha maafisa wa polisi wako karibu na wakazi ili kurahisisha juhudi za kuwahakikishia usalama, huku pia akilalamikia changamoto ya barabara.
“Tuna tatizo la usalama eneo hili ila tunajaribu kulishughulikia kwa njia mbali mbali. Kwanza tunapendekeza kujengwa kituo cha polisi eneo la Ompolion, na pia kujengwa barabara kadhaa ambazo zitafanya rahisi kwa maafisa wa polisi kuendesha doria.” Alisema Ajwang.
Wakiongozwa na machifu wa eneo hilo wakazi walitoa wito kwa serikali kuzidisha juhudi za kuwahakikishia usalama ili pia waishi kwa amani kwani ni kina mama na watoto wanaopitia wakati mgumu kufuatia swala la utovu wa usalama.