WADAU WATAKIWA KUZIDISHA VITA DHIDI YA MIMBA ZA MAPEMA MIONGONI MWA WATOTO WA KIKE.


Jamii imetakiwa kuchangia katika juhudi za kuhakikisha kwamba mimba za mapema miongoni mwa watoto wa kike zinakomeshwa kabisa katika kaunti ya Pokot magharibi.
Ni wito wake naibu mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya Nasokol Dina Mnagat ambaye alisema kwamba mtoto wa kike anafaa kupewa nafasi ya kuendeleza elimu yake ili kuafikia ndoto yake maishani na kuwa na maisha bora ya baadaye.
Mnagat alisema kwamba mimba za mapema zinawapelekea watoto hao kuhangaika maishani kutokana na hali kwamba katika umri huo mdogo hawapo tayari kisaikolojia kutekeleza majukumu ya uzazi, hali ambayo pia inapelekea watoto wanaozaliwa kutopata malezi mema.
“Mimba za mapema si nzuri kwa mtoto wa kike kwa sababu hawajajiandaa kisaikolojia kuwa wazazi na hali hii huwapelekea kuhangaika na hivyo kutowapa malezi mema watoto wanaozaliwa nao. Kwa hivyo watoto hawa wanapasa kupewa fursa ya kuendeleza masomo yao ili pia wanufaike maishani.” Alisema Mnagat
Alitoa wito kwa vitengo vya sheria nchini kukaza kamba dhidi mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi kwa kuhakikisha kwamba wanaopatikana kuhusika na mimba hizo wanachukuliwa hatua kali kwa kuharibu maisha ya baadaye ya watoto hao.
“Vitengo vya sheria vinapasa kukaza kamba dhidi ya visa vya mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi. Wale wanaopatikana kuhusika wanapasa kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa sababu wanaharibu maisha ya baadaye ya watoto hawa.” Alisema Mnagat.