VIONGOZI WATAKIWA KUTOINGIZA SIASA KATIKA ZOEZI LA USAJILI WA WALIMU.


Mbunge wa Kapenguria katika kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Moroto amewataka viongozi wa kisiasa katika kaunti hii kutoingiza siasa katika shughuli ya usajili wa walimu ambayo inaendelea kote nchini.
Moroto alitofautiana na baadhi ya viongozi katika kaunti hiyo ambao wamekuwa wakishinikiza jamii ya kaunti hiyo kupewa kipau mbele katika usajili huo akisema wapo wakazi kutoka jamii zingine ambao wameishi Pokot magharibi miaka yao yote na hawastahili kutengwa katika zoezi hilo.
Alisema kwamba walielewana na tume ya huduma za walimu TSC jinsi ambavyo shughuli hiyo inapasa kuendeshwa na inafaa kupewa nafasi ya kutekeleza majukumu yake kwa njia inayostahili.
“Tumekubaliana huko juu kuhusu jinsi zoezi hilo litaendeshwa na sasa sijui ni kwa nini siasa zinaingizwa kwa shughuli hii. Tunafahamu kipau mbele ni kwa wakazi wa Pokot na ifahamike pia kuna kabila zingine kaunti hii ambazo zimeishi hapa miaka yao yote. Hawa ni wakazi wa kaunti hii na hawapasi kutengwa.” Alisema Moroto.
Moroto alisema kwamba tume hiyo inaendesha shughuli hiyo kulingana na taratibu ilizoweka na hivyo inapasa kupewa muda wa kutekeleza majukumu yake bila miingilio yoyote ya kisiasa.
“Tume ya TSC inapasa kupewa muda wa kufanya kazi yake kitaalam kwa sababu ina mipangilio yake ya jinsi ya kuendesha zoezi hili ili kuhakikisha kwamba watu wote wanaridhika. Kwa hivyo wanasiasa wakae mbali na zoezi la usajili wa walimu.” Alisema Moroto.