DORIA YA KIUSALAMA YAIMARISHWA CHESOGON BAADA YA KUUAWA WATU WAWILI.
Doria imeimarishwa eneo la Chesogon mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo marakwet ili kuimarishwa usalama eneo hilo kufuatia mauaji ya watu wawili na mwingine mmoja kujeruhiwa katika kisa cha uvamizi kilichotekelezwa eneo hilo jumatano wiki hii.
Kamanda wa polisi kaunti hiyo Peter Katam alisema kwamba maafisa zaidi wa usalama wametumwa eneo hilo ili kuhakikisha usalama wa wakazi akitoa wito kwa jamii za eneo hilo kusitisha uhasama na kuishi kwa amani ili kuruhusu shughuli za kawaida kuendelea.
Katam aidha alisema kwamba uchunguzi unaendelea kuhusiana na kisa hicho cha uvamizi kuhakikisha kwamba waliohusika wanakabiliwa kisheria.
“Tumedhibiti vyema eneo hilo na tuna maafisa wa polisi ambao wanaendelea kushika doria. Na ninawahimiza tu wananchi kwamba tudumishe amani kwa sababu mambo ya vita hayatasaidia kwa vyovyote. Uchunguzi unaendelea na wale ambao walihusika na hicho kitendo watachukuliwa hatua za kisheria.” Alisema Katam.
Wakati uo huo Katam aliwaonya vikali wanaomiliki bunduki kinyume cha sheria akisitiza kwamba maafisa wa polisi wanaendeleza uchunguzi kuhusiana na umiliki wa silaha hizo kuhakikisha kwamba zinaondolewa mikononi mwa raia wanaozimiliki bila kibali.
“Natoa onyo kwa wale ambao wanamiliki bunduki kinyume cha sheria kwamba watachukuliwa hatua. Mtu yeyote ambaye amejihami na anatumia bunduki kuwahangaisha watu wengine afahamu kwamba tutamfikia karibuni. Tuna orodha ya wale wanaomiliki silaha hizo na tunawaendea.” Alisema.