WADAU POKOT MAGHARIBI WAENDELEZA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA ATHARI ZA UKAME.
Mashirika mbali mbali ya kijamii kaunti hii ya Pokot magharibi yanashirikiana na serikali ya kaunti katika kubuni mikakati ya kukabili athari ambazo huenda zikasababishwa na ukame ambao unashuhudiwa kufuatia ripoti kwamba huenda hali hii ikaendelea kushuhudiwa kwa muda.
Akizungumza baada ya kikao cha kujadili mikakati hiyo na wadau mbali mbali, mshirikishi wa maswala ya nyanjani katika shirika la action against hunger Salome Tsindori, alisema kwamba kwa ushirikiano na shirika la UNICEF na idara ya afya pamoja na NDMA, wameweka mikakati ya kuhakikisha kwamba miongoni mwa maswala mengine watoto watakaougua utapia mlo wanashughulikiwa.
“Kulingana na ripoti ambayo tumepokea kutoka kwa idara ya utabiri wa hali ya anga ni kwamba huenda kusishuhudiwe mvua hivi karibuni na sasa kama wadau tumeamua kushirikiana na serikali ya kaunti kuhakikisha kwamba tunashughulikia hali. Miongoni mwa mikakati hii ni kuhakikisha watoto watakaougua utapia mlo wanashughulikiwa.” Alisema Tsindori.
Ni kauli ambayo ilitiliwa mkazo na afisa katika shirika la kuangazia maswala ya watoto UNICEF Elizabeth Cherop ambaye aidha alisema kwamba watafikia zaidi watoto katika jamii ambazo zinakabiliwa na changamoto kufikia vituo vya afya kufuatia umbali wa vituo hivyo.
“Tunalenga zaidi watoto kutoka jamii zilizo mbali na vituo vya afya. Huduma zetu nyingi zitakuwa za kutoka nje sana ili kuwafikia watoto walio katika hatari ya kuathirika na utapia mlo. Tunaenda kuwatibu watoto ambao wanaugua utapiamlo kwa kuwapa vyakula vya kuimarisha afya yao.” Alisema Cherop.
Waziri wa utumishi wa umma kaunti hii Martine Lotee alisema kwamba serikali ya kaunti kwa ushirikiano na mashirika haya miongoni mwa mengine, inaendeleza mikakati ya kuhakikisha wakazi pamoja na mifugo wanapata chakula na maji kipindi hiki cha ukame.
“Sisi kama serikali ya kaunti tunashirikiana na mashirika haya kwa lengo la kuhakikisha kwamba wakazi pamoja na mifugo hawahangaiki kutokana na athari ambazo zinasababishwa na ukame hasa baada ya kubainika kwamba huenda tusiweze kushuhudia mvua hivi karibuni.” Alisema Lotee.