RIPOTI YA GIZ YABAINISHA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WAFUGAJI POKOT MAGHARIBI.


Wakulima hasa wafugaji katika kaunti ya Pokot Magharibi wametakiwa kutunza vyema mazingira na kutumia misimu ya mvua kupanda nyasi ya kutosha na aina fulani ya miti ambayo hutumika kama chakula cha mifugo.
Akizungumza katika kikao cha kutoa ripoti iliyoangazia hali ya maisha ya wakazi hasa wanaojihusisha na ufugaji, mkurugenzi wa uzalishaji wa mifugo kaunti hiyo Paul loruchong’ar alisema kwamba hatua hiyo itasaidia wafugaji kustahimili makali ya misimu ya kiangazi kwani watakuwa na chakula kwa ajili ya mifugo yao.
“Nawahimiza wafugaji kuangalia mazingira na kuyatunza. Wafanye mazoea ya kupanda nyasi kwa wingi wakati wa mvua. Wachunge pia hiyo miti ambayo mifugo wanakula kama vile tuyunwo na sesoi. Wasiiharibu ili wakati wa kiangazi wasiweze kuhangaika kutokana na ukosefu wa lishe.” Alisema Loruchong’ar
Wito wake Loruchong’ar unafuatia matokeo ya ripoti hiyo ambayo ilibaini kwamba miongoni mwa maswala mengine, wengi wa wakulima wanakabiliwa na changamoto tele wakati wa kiangazi hali inayowalazimu kuhamia taifa jirani la Uganda kutafuta lishe kwa ajili ya mifugo yao.
“Mara nyingi wakati wa kiangazi lishe ya mifugo huwa tatizo, sasa inabidi wafugaji wahame na mifugo yao hadi taifa jirani la Uganda kutafuta lishe pamoja na maji. Pia kuna tatizo la magonjwa ambalo limesalia changamoto kwa wafugaji hasa misimu ya kiangazi.” Alisema.
Alisema kwamba ripoti ya utafiti huo uliofadhiliwa na shirika la GIZ itasaidia katika kushughulikia changamoto ambazo wafugaji katika kaunti ya Pokot magharibi wanakabiliana nazo kwa lengo la kuimarisha hali ya maisha ya wafugaji na mifugo yao.