VIONGOZI WA MAENEO KAME NCHINI WATOFAUTIANA NA WANAOSHINIKIZA MABADILIKO YA KATIBA.
Shinikizo zikiendelea kutolewa kufanyia katiba ya sasa marekebisho ili kutekelezwa maswala mbali mbali ya uongozi wa sasa, baadhi ya viongozi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamepinga jaribio lolote la kutekeleza marekebisho hayo.
Wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto, viongozi hao walisema kwamba ilivyo kwa sasa katiba hiyo ni bora zaidi hasa kwa wakazi wa maeneo kame nchini kwani imepelekea maeneo haya kuangaziwa sawa na maeneo mengine ya nchi.
Moroto alitaja uongozi wa magatuzi ambao umeletwa na katiba ya sasa kuwa chanzo kikuu cha maeneo kame nchini kuwa sawa na maeneo mengine kwani sasa yamenufaika na mandeleo ambayo yamekuwa yakitekelezwa maeneo mengine ya nchi.
“Hatutaki mtu aguse katiba iliyopo kwa sasa kwa sababu sisi hasa kutoka kaunti za wafugaji na kame tunajua ni vipi imetusaidia. Serikali za magatuzi zimetufanya kuwa sawa na wakenya wengine kwa sababu sasa kaunti hizi zinatengewa mgao wa kutosha kufanikisha shughuli za maendeleo maeneo haya.” Alisema Moroto.
Moroto alisema katiba ya sasa iligharimu kujitolea kwa baadhi ya viongozi nchini akiwemo kinara wa chama cha ODM Raila Odinga kuhakikisha kwamba wakenya wanapata uongozi bora utakaoleta huduma karibu na mwananchi na hivyo haipasi kubadilishwa kiholela.
“Naipongeza hii katiba tuliyo nayo. Na ndiyo maana huwa nasema kwamba kinara wa ODM Raila Odinga alifanya kazi kubwa sana kwa hii nchi na tutaendelea kumheshimu kwa nafasi yake. Tunatambua sana juhudi zake ambazo zilipelekea kuwepo katiba ya sasa na hatutaruhusu mtu aifanyie mabadiliko kiholela.” Alisema.