WAFANYIBIASHARA MJINI MAKUTANO POKOT MAGHARIBI WALALAMIKIA KUKITHIRI WIZI.


Wafanyibiashara mjini makutano katika kaunti hii ya Pokot magharibi wametakiwa kuwa waangalifu hasa msimu huu ambapo visa vya wizi vimetajwa kukithiri.
Hii ni baada ya wasichana wawili kunaswa hiyo jana wakijaribu kuiba nguo na viatu kutoka kwenye duka moja mjini humo.
Wakiongozwa na Frankline Momanyi wafanyibiashara walielezea kukadiria hasara kufuatia kukithiri visa vya wizi katika mji wa Makutano katika siku za hivi karibuni.
“Wizi umekithiri sana mjini Makutano hasa kwenye steji. Tumekuwa tukikadiria hasara sana kutokana na kuongezeka wizi. Nawaomba wafanyibiashara wote makutano wawe makini sana wakati huu.” Alisema Momanyi.
Wafanyibiashara hao sasa wanatoa wito kwa idara ya usalama kuimarisha usalama katika mji huo na pia kuhakikisha kwamba wanaokamatwa wakihusika katika wizi wa bidha wanachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Hili swala la wizi sasa tumechoka nalo. Tumeibiwa mara si moja. Kwa hivyo naiomba serikali kuongeza ulinzi kwa wafanyibiashara wote mjini Makutano na pia kuhakikisha kwamba wanaokamatwa wakihusika wizi wanachukuliwa hatua.” Walisema.
Ni kisa kinachojiri siku chache baada ya kamanda wa polisi kaunti ya Pokot Magharibi Peter Katam kutoa hakikisho kwamba maafisa wa polisi wataimarisha doria maeneo yote ya kaunti hiyo ikiwemo ya kibiashara kuhakikisha kwamba wahalifu hawatumii msimu huu kuendeleza vitendo vyao vya kihalifu.
Aidha Katam aliwataka walinzi wa maeneo ya kibiashara kuwa makini msimu huu akionya kwamba mlinzi yeyote atakayetelekeza majukumu yake atawajibishwa iwapo wizi utatokea eneo ambalo anawekea ulinzi.