HOSPITALI YA ORTUM YACHUNGUZWA KUHUSIANA NA KISA CHA KUNYOFOLEWA BAADHI YA VIUNGO VYA MTOTO ALIYEZALIWA AKIWA TAYARI AMEFARIKI.
Hospitali ya kimisheni ya Ortum katika kaunti hii ya Pokot magharibi inachunguzwa kufuatia kisa ambapo baadhi ya viungo vya mwili wa mtoto uliohifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo vilikuwa vimeondolewa.
Akithibitisha kisa hicho kamanda wa polisi kaunti ya Pokot magharibi Peter Katam alisema mkazi mmoja alimpeleka mkewe katika hospitali hiyo kujifungua ila mwanawe akatoka akiwa tayari amefariki na mwili wake kuhifadhiwa katika hospitali hiyo ambako inaaminika ulitenganishwa na kichwa.
“Kuna mama aliyefika katika hospitali ya Ortum kujifungua ila mtoto akatoka akiwa tayari amefariki na wakamweka katika chumba cha kuhifadhi wafu. Ila baadaye walipofika kuuchukua mwili ili kuuzika wakapata mwili umetenganishwa na kichwa na haupo. Tunafuatilia kisa hicho ili tubaini ni nini kilichotokea.” Alisema Katam.
Katam alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa akina mama wajawazito kufanya mazoea kutafuta huduma za vituo vya afya ili kuhakikisha kwamba mtoto anasalia salama hadi wakati wa kujifungua ili kuzuia visa vya watoto kuzaliwa wakiwa wameaga dunia.
“Nawahimiza kina mama kuwa na mazoea ya kufika katika vituo vya afya wanapokuwa wajawazito kukaguliwa kila mara na wahudumu wa afya ili kupunguza visa vya watoto kuaga dunia wakiwa hawajazaliwa.” Alisema Katam
Wakati uo huo Katam alisema kwamba polisi wanaendesha uchunguzi kuhusiana na kisa cha kupatikana kichwa cha binadamu karibu na mto Arabi kata ya Batei eneo hilo la Ortum kikiwa ndani ya mfuko pamoja na simu.
“Tulipata ripoti kutoka kwa chifu wa Batei huko Ortum kwamba kulikuwa na kichwa cha mtu kilichokuwa karibu na mto wa Arabi. Maafisa wa polisi kutoka kituo cha Ortum walipofika eneo hilo wakapata kichwa katika mfuko pamoja na simu. Sasa hatujui nini kilifanyika hadi kichwa kikapatikana eneo hilo.” Alisema.