SHINIKIZO ZAENDELEA KUTOLEWA KWA RAIS KUTIMIZA AHADI ZAKE KWA WAKENYA.
Zaidi ya siku 100 tangu rais William Ruto kuingia afisini, shinikizo zimeendelea kutolewa kwake kuhakikisha kwamba anatekeleza ahadi alizotoa kwa wananchi kwamba angetekeleza ndani ya siku hizo 100 baada ya kuingia afisini.
Baadhi ya wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi wameelezea kukumbwa na hali ngumu kufuatia kupanda gharama ya maisha wakielezea kudorora hali ya usalama inayosababishwa na baadhi ya vijana ambao wamekosa ajira baada ya kusitishwa mpango wa kazi kwa vijana.
Aidha wakazi hao walimtaka rais Ruto kutoa fedha zilizotengewa makundi mbali mbali hasa wazee ambao wamesema kwamba wanapitia changamoto tele kufuatia kutotolewa fedha hizo kwa zaidi ya miezi mitano sasa.
“Rais aliahidi mambo mengi akisema kwamba ndani ya siku 100 ataleta mabadiliko. Na sasa uchumi wa Kenya umekuwa mbaya zaidi. Wakulima wanalia, vijana hawana kazi na sasa kazi ya vijana ambayo ilikuwa inawasaidia ilisimamishwa. Wazee pia wanangaika kwa kusimamishwa pesa zao kwa miezi mitano sasa.” Walisema.
Wakati uo huo wakazi hao walimtaka rais Ruto kuongeza kiwango cha mikopo inayotolewa kupitia hazina ya Hustlers fund wakisema kwamba fedha zinazotolewa kwa sasa ni kidogo mno na haziwezi kumsaidia mtu kuanzisha biashara.
“Pesa za hustlers fund ambazo zinatolewa sasa hazitoshelezi mahitaji ya wafanyibiashara kwa sababu ni kidogo sana. Tunamtaka rais Ruto kuongeza pesa hizo ambazo alisema kwamba zinanuia kuinua mtu wa chini kabisa. Pesa hizo hazisaidii huyu mwananchi.” Walisema.