MIKUTANO YA AZIMIO YAUNGWA MKONO NA WAJUZI WA SHERIA POKOT MAGHARIBI.

Baadhi ya wajuzi wa maswala ya kisiasa katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameunga mkono mikutano ya umma ambayo inatarajiwa kuandaliwa na chama cha muungano wa azimio la umoja one Kenya kuanzia Jumatano.

Wakiongozwa na wakili Eric Chang’rok, wajuzi hao wa maswala ya kisiasa walisema kwamba ni jukumu la kisheria kwa chama chochote cha upinzani kuiwajibisha serikali iliyo mamlakani na hivyo ni haki kwa muungano wa azimio kuandaa mikutano hiyo anayosema ni dhihirisho la kuwajibika upinzani nchini.

“Hii ni njia moja ya kuhakikisha wakenya wanapata huduma kutoka kwa serikali na kuiwajibisha serikali kufuatia ahadi zake. Hii ni kazi ya upinzani kulingana na sheria. Upinzani ukinyamaza na kuiachia serikali nafasi, maovu yataendelea kushuhudiwa serikalini.” Alisema Changrok.

Hata hivyo Chang’rok alielezea wasi wasi wa kuwepo upinzani dhaifu nchini kutokana na hali kuwa baadhi ya vyama tanzu katika muungano wa azimio vimeendelea kujiondoa cha hivi punde kikiwa chama cha KUP kinachoongozwa na aliyekuwa gavana wa Pokot magharibi John Lonyangapuo.

“Serikali ina wabunge wengi na hata vyama ambavyo vilikuwa upande wa upinzani vimeanza kujitoa na kujiunga na serikali. Hii inaashiria huenda wananchi wakasalia bila upinzani wenye nguvu wa kuiwajibisha serikali. Wabunge watapata wanachotaka kwa serikali ila mwananchi wa kawaida ataumia.” Alisema.

Kulingana na Chang’rok huenda chama hicho cha KUP kikajiunga na serikali ya Kenya kwanza, hatua anayosema kwamba haifai kuathiri majukumu ya wabunge wa upande wa upinzani katika bunge la kaunti ya Pokot magharibi.

“Ukiona kiongozi amefika kiwango cha kutangaza hivyo, kuna uwezekano kwamba amekutana au ana mpango wa kukutana na serikali na kufanya kazi nayo. Ila hatua hii haifai kuathiri wabunge wa upinzani katika bunge la kaunti hii. Upinzani unafaa kuendelea kuiwajibisha serikali ya kaunti.” Alisema.