VYAMA VYA USHIRIKA POKOT MAGHARIBI VYALENGA KUANZISHA UPANZI WA MACADAMIA, KUBORESHA KILIMO BIASHARA.

Kama njia moja ya kuinua na  kuboresha kilimo cha kahawa, vyama vya ushirika kaunti  hii ya Pokot Magharibi kupitia mwenyekiti wao Samson kamarich vimesema kuwa wana nia ya kuanzisha upanzi wa macadamia.

Kulingana na Kamarich hatua hii ni njia moja ya kuinua kilimo biashara hasa kwa wakulima ambao wanakuza kilimo cha kahawa.

“Tunatarajia kuanza upanzi wa mmea wa macadamia ambao tulipewa mapema mwaka huu na serikali ya kaunti lengo letu kuu likiwa kuimarisha kilimo biashara katika kaunti hii ya Pokot magharibi hatua itakayopelekea manufaa kwa mkulima wa kahawa.” Alisema Marich.

Akizungumza katika mahojiano na kituo hiki Marich alisema kwamba kwa sasa wanaendeleza mikakati ya kuhakikisha wakulima wanapata elimu ya jinsi ya kukuza mmea huo pamoja na sehemu ambako watapata soko la mazao yao.

“Tunaweka mikakati ya kutoa mafunzo kwa wakulima wetu jinsi ambavyo watapata mmea huu, jinsi watakavyoukuza na sehemu ambako watapa soko.” Alisema.

Ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wazazi katika kaunti hii kuwahusisha wanao katika shughuli mbali mbali ikiwemo za shambani kabla ya shule kufunguliwa mwakani, ili kuwazuia kujihusisha na vitendo vilivyo kinyume na maadili hasa msimu huu wa sherehe nyingi.

“Watoto wasikae bure nyumbani na kupata mawazo ya kujihusisha na tabia zisizoridhisha. Wazazi wawahusishe katika shughuli za shambani kama vile kuvuna kahawa na kukusanya mbolea inayotokana na mifugo na kuweka shambani.” Alisema.