MBUNGE WA SABOTI ATAKA KUBUNIWE HAZINA YA USTAWISHAJI MAENEO YA WADI.

Mbunge wa Saboti katika kaunti ya Trans nzoia Caleb Amisi amesema kwamba atahakikisha waakilishi wadi wanapokea fedha za ustawishaji maeneo wadi kutoka kwa serikali ya kaunti katika juhudi za kuhakikisha kwamba miradi ya maendeleo inaafikiwa maeneo ya mashinani.

Amisi alisema kwamba waakilishi wadi wanastahili kupokea fedha za kustawisha maeneo yao ya utawala jinsi ilivyo kwa wabunge wanaopokea mgao wa NGCDF akisema kwamba kwa sasa viongozi hao wa maeneo ya mashinani wanapokea fedha kidogo ambazo haziwawezeshi kuafikia lolote.

“Kwa sasa waakilishi wadi wanapokea fedha kidogo sana ambazo haziwawezeshi kutekeleza maendeleo inavyohitajika katika maeneo ya mashinani. Naahidi kuhakikisha kwamba waakilishi wadi kaunti hii ya Trans nzoia na taifa kwa jumla wanapokea fedha za kutosha jinsi ilivyo kwa wabunge.” Alisema Amisi.

Akizungumza katika ibaada ya jumapili kwenye kanisa moja eneo la Lukhome wadi ya machewa akiandamana na waakilishi wadi wote wa eneo bunge la Saboti, Amisi aidha alisifia ushirikiano mwema uliopo baina ya waakilishi wadi hao na gavana George Natembeya hatua anayosema itasaidia kuimarisha maendeleo.

“Ushirikiano uliopo kwa sasa baina ya waakailishi wadi katika kaunti hii ya Trans nzoia na gavana George Natembeya ni wa kuridhisha ikilinganishwa na utawala uliotangulia. Hatua hii bila shaka itawezesha kuafikiwa maendeleo yanayohitajika kwa watu wetu kaunti hii.” Alisema.